AGIZO: Waziri Mwakyembe aivaa Startimes.. #share.. aiundia 'kikosikazi' cha watu kumi...


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Dk. Harrison Mwakyembe amesema ameunda kamati ndogo ya watu 10 kuhusiana na agizo la Rais Magufuli la Kampuni ya Star Media, ambapo majibu yatapatikani ndani ya siku saba.


Akizungumza Dar es Salaam, leo baada ya kumaliza kikao na Mwenyekiti wa kampuni hiyo Xinxing Pang, alisema baada ya agizo la Rais walikaa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TCRA) pamoja na wizara yake kupitia masuala mbalimbali ndipo walipofikia uamuzi wa kuunda kamati.

Alisema kamati hiyo imeundwa na watu watano kutoka Tanzania na watano kutoka kwao, ambapo kwa kipindi hicho naye Mkaguzi Mkuu wa Hesababu za Serikali (CAG) alikuwa anamalizia uchunguzi wake.

“Sula hili hatutaki lichukue muda mrefu, tunataka liishe mwezi huu, ambapo majadiliano yatakayopatikana kwenye kamati hiyo nitampigia simu Mwenyekiti kumueleza tulipofikia. Kwa sababu tayari sisi tulikuwa na msimamo wetu.

“Ndiyo maana aliamua kuja kutoka China ili kujua moja kwa moja kuhusiana na msimamo wetu na kuwa kwa nini Kampuni yao haileti faida,”amesema Dk. Mwakyembe.

Alifafanua kuwa makubaliano hayo ya kuunda kamati yalifikia baada ya kukaa nao katika mazungumza na wao wakatoa sababu zao ndipo walipofikia uamuzi huo wa kamati ili kujua nini ambacho kinasababisha faida isipatikane.

Alibainisha kuwa kwa hatua hiyo agizo la Rais Magufuli limefanyiwa kazi na wakishamaliza kushughulikia suala hilo watampelekea taarifa rasmi za uchunguzi wa kina.

Hata hivyo, akifafanua kuhusu ripoti ya CAG alisema wanategemea kupata ripoti hiyo muda wowote kuanzia sasa, hata wao bado hawajaisoma, kwa sababu wanataka jambo hilo lifanyiwe kazi haraka waliamua kufanyia kazi mkataba wa makubaliano.

“Tunataka jambo hili limalizike mapema ndiyo maana tukaamua kushughulika kwanza na mkataba na hiyo ripo ya CAG yenyewe itasaidia yale majadiliano yatakayopatikana kwenye kamati ndiyo maama tumeipa kamati siku saba tu,”alisema

Dk. Mwakyembe alisema kama timu hiyo haitamaliza kazi yao kwa wakati kwa kudhani kuna suala la msingi imeliacha, itaongezewa siku mbili au tatu iweze kulikamilisha kutokana na umuhimu wa suala hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti huyo, amesema amekuja nchini kwa sababu ya maswali kadhaa yaliyotolewa na Rais Magufuli kutokana na Kampuni yao, kwa hiyo wamezingatia maswali hayo na watayafanyia kazi.


“Tunafanya juhudi nyingi za kujibu maswali hayo na ndiyo maana nimekuja kuzungumza na Waziri na kutoa  mrejesho wa kazi tuliyofanya za Star Media na pia tunatafuta sababu ambazo Kampuni yetu inatupa hasara na njia ya kutupa faida baadaye,” alisema
Na Abraham Ntambara

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search