MORNING TALK.. Mastaa wa Premier League Uingereza walivyoipaisha Tanzania.. sasa ndio Nchi Bora kiutalii Afrika.. Yussuf Manji akimbizwa JKCI Hospital.. Watanzania 48,695 wameshafariki kwa ajali tuu.. #share.. Aliejiuzulu Ujaji sasa ni Marehemu.. Stars yasema 'ni mwendo wa ushindi Rwanda..'

Wakati idadi ya watu maarufu kutoka nje ya nchi wanaokuja kutazama vivutio vya utalii nchini ikiongezeka, mtandao wa kimataifa wa kibiashara umeitangaza Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika inayowavutia zaidi watalii.


Mtandao huo, SafariBookings.com ulifanya uchambuzi kwa kuchukua maoni ya watalii zaidi ya 2,500 waliotembelea nchi za Afrika na idadi kubwa waliitaja Tanzania kuwa bora kuliko nchi nyingine.

Hii ni mara ya pili kwa mtandao huo wa Marekani kuitaja Tanzania kama nchi ya kwanza inayowavutia zaidi watalii. Mara ya kwanza ilikuwa 2013.

Sifa kubwa iliyoipa hadhi ya juu Tanzania ni kuwa na eneo kubwa lenye wanyamapori na misitu. Nchi nyingine zilizoshika nafasi ya juu ni Zambia na Kenya.
Wakati mtandao huo ukiitaja Tanzania kuwa eneo bora la utalii, watu maarufu kutoka mataifa makubwa duniani wameendelea kumiminika nchini wakitembelea hifadhi za Taifa na vivutio vingine.

Miongoni mwa watu maarufu waliotembelea vivutio hivyo ni pamoja na mwanamuziki wa Marekani, Usher Raymond na mcheza soka maarufu David Beckham aliyewahi kuchezea timu ya Taifa ya England na timu za Manchester United na Real Madrid.

Mara baada ya kutembelea vivutio hivyo, Usher aliweka picha za ‘matanuzi’ aliyopata akiwa Tanzania, katika mitandao yake ya kijamii ya Twitter na Instagram.

Usher alikuwa ameongozana na familia yake wakiwamo watoto wake wawili wa kiume katika Hifadhi ya Serengeti.
“Safari hii imekuwa ya maajabu, tumefurahi sana kuona uzuri wa mbuga hii nikiwa na familia yangu,” ameandika katika ukurasa wake wa Twitter.


Si hao tu, watu wengine maarufu waliofika ni mcheza filamu wa Marekani, Will Smith na familia yake na mchezaji wa zamani wa timu ya Liverpool, Mamadou Sakho.

Pia, mchezaji wa Everton Morgan Schneiderlin alitembelea vivutio hivyo hivi karibuni akiwa fungate.

Wiki hii, msanii maarufu wa filamu za Bolywood, India, Sanjay Dutt naye aliwasili kwa ajili ya kutembelea vivutio hivyo.

Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limesema kazi kubwa inayofanywa na shirika hilo kutangaza vivutio vya utalii duniani ndiyo iliyozaa matunda hayo.

Msemaji wa Tanapa, Paschal Shelutete alisema lengo lao ni kufikia watalii milioni tatu ifikapo mwaka 2020. Alisisitiza kwamba Tanapa inatathmini namna ya kuwatumia watu mashuhuri wanaotembelea nchini kujitangaza zaidi kimataifa ili kufikia lengo hilo.

Alipoulizwa namna wanavyoitumia fursa ya watu hao mashuhuri kutembelea nchi, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Phillip Chitaunga alisema, “Hili ni jambo ambalo kwetu tunalichukulia kwa mapana yake kwa sasa.”

Akizungumzia vivutio vilivyopo nchini, mwandishi wa habari za usafiri na utalii wa Marekani, Tim Bewer alisema, “Tanzania ina Mbuga nyingi nzuri kama Serengeti na Ngorongoro, wanyama watano bora, simba wapandao miti, kikubwa ni ubora wa hifadhi hizo ambazo zimetumia robo tatu ya ardhi yake kuhifadhi wanyamapori.”

Pia, mtaalamu wa masuala ya safari na utalii na raia wa Uingereza, Phillip Biggs amekaririwa na jarida mtandao la Huffpost akisema, “Hakuna majadiliano, hakuna nchi ya Afrika, kusema ukweli, yenye wanyama wakubwa katika eneo kubwa kama Tanzania.” - mwananchi online

======================================

JUMLA ya watu 48,695 wamekufa na wengine 282,194 kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani zilizotokea nchini Tanzania katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi 2015.

Uchunguzi wa jarida moja la kimtandao la fikraperu umeonyesha kwamba, katika kipindi hicho cha miaka 16, jumla ya ajali 302,875 zilitokea na kati ya hizo ajali mbaya zilizosababisha majeruhi na hata vifo zilikuwa 41,690.






Kwa mujibu wa uchunguzi huo, idadi hiyo ya ajali ni wastani arwa ajali 18,930 kwa mwaka ambayo pia ni wastani wa ajali 52 kwa siku.

Aidha, jarida hilo pia limebaini kwamba, wastani wa watu 10 hufariki dunia kila siku nchini Tanzania kutokana na ajali hizo.
Taarifa kutoka Ofisi ya taifa ya Takwimu pamoja na Jeshi la Polisi zinaeleza kwamba, mwaka 2013 ndio uliokuwa na majanga kutokana na kurekodi jumla ya ajali 24,480 ambapo kati ya hizo, ajali mbaya zilikuwa 3,545 ambazo zilisababisha vifo 4,091... soma zaidi kwenye kiunganishi chini

=========================================
Kocha msaidizi wa timu ya Taifa stars, Fulgence Novatus amesema atahakikisha timu yake inapata ushindi katika mechi yao ya marudiano dhidi ya Amavubi ya Rwanda kwa madai wameyafanyia kazi mapungufu waliyokuwa nayo.
kikosi kamili cha Stars kilichoelekea mjini kigali, Rwanda.
Novatus ameeleza hayo wakati kikosi chake kikiwa kinajiandaa na safari ya kwenda mjini Kigali, Rwanda kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Amavubi katika kuwania tiketi ya kucheza fainali za kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN 2018) zitakazofanyikia Kenya.

"Tumeyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo wetu wa kwanza dhidi ya wapinzani wetu Rwanda katika uwanja wa 'Stade de Kigali', wachezaji wote ni wazima isipokuwa Shomari kapombe ambaye aliumia wakati wa mechi ya kwanza. Naamini timu yangu itaibuka na ushindi ili iweze kufuzu kucheza fainali za kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN 2018)", amesema Novatus.

Pamoja na hayo, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda amesema kwamba wamekifanyia mabadiliko machache kikosi hicho ili waweze kupata ushindi katika mechi hiyo ya marudiano.

"Tumefanya mabadiliko na sasa Taifa Stars ya kocha Salum Shaaban Mayanga itaondoka Jumatano badala ya Alhamisi, ili kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji pamoja na hali ya utulivu wakiwa nchini Rwanda kabla ya mchezo huo", amesema Lucas.
Kwa upande wake Nahodha wa Taifa Stars Himid Mao amewaomba watanzania kwa ujumla waungane na kuiombea timu yao iweze kutimiza malengo yao ya kufuzu kucheza michuano ya wachezaji wa ligi za ndani(CHAN).

======================================



















About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search