nEWS: 'Spika Makinda' anga'ra uzinduzi 'toto card' NHIF.. Waziri Ummy atoa neno kwa wazazi kukata bajeti ya 'vilevi'.. afya ya mtoto ndio mtaji.. #share..

JAMII nchini imeshauriwa kuacha tabia ya kutumia fedha kwenye masuala yasiyo na ulazima badala yake ijikite katika kuitumia fedha kuwekeza kwenye bima ya afya kwa ajili ustawi wa afya na maendeleo ya nchi.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa Uzinduzi wa Bima ya Afya ya Mtoto iliyopewa jina la Toto Afya Kadi inayolenga kumsaidia mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 kupata huduma za afya.
Alisema jamii hasa hasa wazazi wamejenga utamaduni kutumia fedha kwenye mambo hayana faida kwao huku akisisitiza fedha nyingi hutumiwa katika uchangiaji sherehe na matumizi ya vilevi bila kujali kuwekeza afya zao na watoto.
" Mtu akikaa baa anatumia hadi sh 100,000 kwa kuzungusha raundi ya bia ni bora hiyo hela akaiweka kwenye mfuko wa bima ya afya kwa ajili yake na watoto wake," alisema Ummy.
Waziri Ummy alisema sio wananume pekee wanatumia fedha kwenye vilevi huku akibainisha hata wanawake hutunzana kiasi kikubwa cha fedha wakisahau umuhimu wa bima ya afya za watoto wao.
Aliuomba Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wazazi hawana uwezo kulipa Sh 50,400 ya kadi hiyo kwa mara moja na kwamba walipie kwa kipindi cha awamu tatu au nne kwa miezi mitatu wawe wamemaliza kisha wapatiwe kadi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bernard Konga amesema hadi sasa wameshasajili watoto 50,000 wa mkoani humo na wana mpango endelevu wa kusajili watoto wengi zaidi kupitia ofisi zao za mikoani ambapo kampeni yao imelenga kuzifikia sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu mbalimbali ikiwemo sehemu za ibada na sokoni.
Pia ameeleza kuwa katika Sikukuu ya Nanenane watakuwa na mabanda ambayo yatatumika kusajili na hivyo wazazi wanatakiwa kwenda na vyeti vya kuzaliwa vya watoto wao na picha ndogo (Passportsize) na kiasi cha Sh 50,400.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Anne Makinda amewataka watoa huduma wa vituo vya afya, hospitali na zahanati kuacha kutumia lugha ya matusi kwa wanaotumia kadi za bima za afya.
Ameahidi kutekeleza agizo la Waziri Mwalimu kuhusiana ulipaji wa awamu wa kadi hiyo na uanzishwaji wa Bima ya Mzazi na Mwana ifikapo mwezi Disemba.
Makinda ameishukuru Hospitali ya TMJ kwa kuwalipia watoto 100 huku Hospitali ya Regency ikiwalipia watoto 120 kadi za bima za afya zitakazogawiwa kwa watoto wenye mazingira magumu.
No comments:
Post a Comment