NEWS: Zitto awashukia wanaomkejeli kwa kusifia utendaji wa JPM.. #share
Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa chama
cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amewajibu baadhi ya watu wanaomkosoa na kumuita
msaliti kutokana na kitendo cha kumsifia Rais John Magufuli alipokuwa ziarani
katika jimbo lake.
Rais Magufuli akiwa na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe alipofanya ziara jimboni kwake hivi karibuni.
Zitto amewajibu watu hao leo wakati akizungumza na wananchi
wa Kigoma Mjini, amesema asingeweza kumkosoa Rais Magufuli kwa kuwa alikuwa
mgeni jimboni kwake na pia alikuwa anafanya shughuli za maendeleo ya wananchi
wa jimboni kwake.
“Rais alikuja hapa akafungua mradi
wa maji tukaenda ziwa Tanganyika, kuna watu walikasirika sababu Rais alinisifia
sana, hawezi akaja Kigoma mtu akanisema mimi vibaya mkakubali na mgeni akija
siwezi nikaanza kumsema vibaya,”
“Mgeni akija unamkaribisha
anafanya kazi yake anaondoka, kwani rais akienda kwenye majimbo yao wanamsema,
rais alikwenda Bukoba Mjini wakati wa tetemeko, mbunge wa jimbo hilo alimsema ?
alikwenda Arumeru kwa mdogo wangu Joshua Nasari, alimsema rais kwa nini akija
kigoma mimi ndio nimseme,” alihoji Zitto.
Aliongeza kuwa “Mimi
hamkunifundisha kuwa mazwazwa wazee mlinifundisha adabu na kuhakikisha
maendeleo yanapatikana lakini sio kwamba rais akikosea hatutamsema tutamsema,
na tumeshamsema sana, sisi ndio chama cha mwisho kufanya mkutano wa ziara,
tukaja operesheni ya linda demokrasia tumemaliza mikutano ikapigwa
marufuku.”
“Lakini toka serikali ya awamu ya
tano iingie madarakani uhuru umeanza kuminywa sasa ni lazima, hatuwezi kukaa
kimya haki ya watu kuwa na mawazo tofauti hatuwezi kuikalia kimya hata kidogo,
lakini wakati huo huo hatuwezi tukasimamisha kila kitu kusubiri haki ya kuwa na
mawazo huru, lazima haki ya mawazo huru ipiganiwe wakati tunapigania
maendeleo,” amesema
Chanzo: MO.
Blog/ Regina Mkonde
No comments:
Post a Comment