gOOD nEWS: Dawasco yaja na huduma ya maji kwa njia ya simu....#share
KATIKA kuhakikisha inarahisisha upatikanaji wa huduma ya
maji safi na kwenda na mfumo wa kisasa wa mawasiliano ya kiteknolojia, Shirika
la MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) limezindua mfumo mpya wa
mawasiliano ambao unalenga kumrahisishia mteja kupata na kutoa taarifa zinazohusu
huduma hiyo kwa haraka Zaidi.
Meneja Uhusiano wa Dawasco,
Bi. Everlasting Lyaro (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na
Teknolojia wa DAWASCO Bwana Kiula Kingu.
Huduma hiyo mpya sasa itapatikana kwa wakazi wote wa jiji la
Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Mkurugenzi
wa Mawasiliano na Teknolojia (TEHAMA) wa Dawasco, Kiula Kingu amesema lengo kuu
la mfumo huu ni kumweka mteja karibu kihuduma na kila mwananchi ana uwezo wa
kutumia mfumo huo katika simu yake kupitia mitandao yote ya simu za mikononi
nchini.
Kingu ameongeza kuwa ili mteja kunufaika na mfumo huu anatakiwa kuhakikisha ana simu ya mkononi ya 'Smartphone' ambayo itamwezesha kupakua mfumo huo mpya wa DAWASCO, kisha kujisajili kwa kuingiza akaunti namba yake ya DAWASCO ambapo baada ya kufuata hatua zote za kujisajili mteja atatumiwa neno la siri ambalo litamwezesha kuingia na kupata taarifa husika.
“Sisi Dawasco tumeona haja ya
kujiboresha na kwenda sawa na teknolojia kwa kumletea mteja wetu mfumo rahisi
ambao utamwezesha kupata taarifa zetu kupitia simu yake ya mkononi muda
wowote,”amesema Kingu.
Naye, Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Everlasting Lyaro,
amewataka wananchi wa Dar es Salaam na Pwani kupakua mfumo huu kwani ni rahisi
kuutumia na hauna gharama zozote.
Amesema ni mfumo ambao utamrahisishia mteja kupata taarifa
muhimu zinazohusu huduma ya maji zikiwamo ankara ya mwezi, taarifa za lini
mteja alifungiwa huduma ya maji, muda ambao alifanya malipo, lini mita yake ya
maji ilisomwa na taarifa nyingine nyingi.
Na Abraham Ntambara
No comments:
Post a Comment