tREANDING nEWS: Mbowe 'aikalia Kooni' serikali, aituhumu kusababisha maisha magumu kwa Watanzania...#share

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) , Freeman Mbowe amesema maisha ya Watanzania leo ni magumu kuliko wakati wa awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.


Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alikosoa kauli za Serikali kuwa uchumi unakuwa akisema uchumi huo unakuwa katika mifuko ya kikundi cha watu wachache.

Mbali na suala hilo, Mbunge huyo wa Hai ameishutumu Serikali ya CCM kwa matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha za walipa kodi ambazo zitatumika katika chaguzi katika kata ambazo Madiwani walijiuzulu.

Amesema hayo leo wakati akihutubia wakazi wa kijiji cha Shirinjoro katika jimbo la Hai Mkoani Kilimanjaro , Mbowe amesema hali ya maisha ya Watanzania ni mbaya kuliko kipindi cha Kikwete na kwamba kipato cha mwananchi kimeshuka.

“Serikali inasema uchumi unakuwa, tukiwauliza ni viashiria gani vinawafanya muone uchumi unakuwa wanakwambia tumenunua ndege tano na tunajenga reli ya kisasa,”amesema na kuongeza;

“Kama uchumi unakua basi unakua katika mifuko ya kikundi cha watu wachache na sio Watanzania tunaowafahamu ambao maisha yamekuwa magumu kuliko wakati wa Kikwete.”

Mbowe ametumia fursa hiyo kuwahoji wananchi ni kipindi gani maisha ni magumu kati ya utawala wa Kikwete (2005-2015) na wa Rais John Magufuli na kujibiwa kuwa ni wakati wa Magufuli.

Kwa mujibu wa Mbowe, wakati Serikali ikijitapa kukuza uchumi, lakini hali ya maisha kwa Mtanzania imekuwa ngumu kutokana na kushuka kwa kipato na kupanda kwa gharama za maisha.

Mbowe alitolea mfano kuwa wakati uchaguzi ukifanyika mwaka 2015, kilo moja ya sukari ilikuwa Sh1,600 lakini sasa imepanda na kufikia karibu Sh3,000 vivyo hivyo kwa bidhaa nyingine muhimu.

Mbali na suala hilo, lakini amezungumzia hatua ya madiwani wake watatu kujiuzulu na kujiunga na CCM, akisema uchaguzi wa marudio utatafuna kodi za walipa kodi zaidi ya Sh750 milioni.

“Mwaka 2015 katika kata yenu mlimchagua Mzee Kimath (Ernest) lakini ni jambo la aibu CCM kupitia mkuu wa wilaya ya Hai (Gelasius Byakanwa) wanarubuni madiwani wetu,”amesema Mbowe.

“Haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa sababu gharama za kurudia uchaguzi hapa kata ya Mnadani pekeee ni Sh250 milioni. Hizi zingeweza kweda kujenga mashule na zahanati,”amesisitiza.

“Serikali inaona kuliko kuwe na diwani wa upinzani bora turudie uchaguzi kwa gharama ya mamilioni. Nataka niwaambie nitalala hapa Shirinjoro tukirudia uchaguzi na haiendi popote,”amesema.

Mbowe alitumia mkutano huo kuwaeleza wananchi hao kuwa ataendelea kupigania haki za Watanzania hata kama kwa kufanya hivyo atapelekwa gerezani akisema magereza yametengenezewa wanadamu.

“Tunaifanya kazi hii kwa maumivu makubwa ya kifamilia. Tunaifanya kazi hii kwa maumivu makubwa ya kibiashara na kisiasa. Wanadhani wanatunyong’onyeza  lakini wanatuimarisha,”alisema.

“Kazi ya mageuzi ni ya muda mrefu na sio kazi ya masikhara . Ni kazi ya wito inayohitaji uvumilivu. Kama unaroho ndogo huwezi kuwa mpinzani Tanzania. Mimi nimejitoa kwa ajili ya Watanzania”.

“Hawatazuia nguvu ya mageuzi ndio maana hata Rais ana hofu, hajiamini kuwa amekuwa Rais. Hakuna mikutano ya kisiasa tukutane 2020 wakati yeye kila siku anapiga siasa,”alisema Mbowe.

“Sitakaa kimya na siku nikikaa kimya nitakuwa kaburini. Magereza ni jambo la kawaida. Viongozi wa Serikali wanajifanya miungu watu. Akina Mbowe tukinyamaza mtapigwa viboko barabarani,” amesisitiza.

Na Mwandishi Wetu.





About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search