nEWS: ATCL kubeba mizigo na vifurushi vya TPC.....#share

SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL) limeingia mkataba wa miaka miwili wa Makubaliano ya ushirikiano ya kutoa huduma na Shirika la Posta nchini (TPC) wenye lengo la kuboresha huduma zitolewazo na shirika hilo.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema wameamua kusaini mkataba huo na shirika la posta kwa kuwa shirika hilo tayari lina wigo mpana wa utoaji huduma huku akisisitiza watatumia baadhi ya ofisi za TPC kufanikisha shughuli zao.

“Tunasaini makubalinao ya kutoa huduma na Posta kutokana wenzetu tayari wameshajijenga wana vituo vingi vya utoaji huduma tunaamini mizigo na vifurushi havitatumia muda mwingi kufika mahali husika,” amesema Matindi.

Amesema watashirikiana na shirika hilo kwenye masuala ya masoko na biashara huku akibainisha TPC tayari wana mtandao mpana ambao utaifaidisha ATCL.

Amesisitiza kuwa kwa sasa shirika hilo linatoa huduma ya usafiri kuelekea mikoa ya Dodoma, Tabora, Kilimanjaro, Mtwara, Mbeya, Tabora, Mwanza huku akiongeza kupitia ushirikiano huo itasaidia huduma kufika haraka kwenye mikoa inayopakana.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPC, Deo Kwiyukwa alisema baada ya kusaini mkataba huo wateja wanaotumia huduma ya posta wataweza kusafirisha mizigo na vifurushi kwa kutumia ndege za ATCL kwa gharama nafuu.

Kwiyukwa amesema wafanyakazi wa TPC watatumia huduma ya shirika hilo pale panapohitajika kutoka sehemu kwenda nyingine yote katika kuharakisha huduma kwa wateja.

Amefafanua kuwa mkataba huo una tija kwa kuwa utasaidia kuongeza usalama wa mizigo na vifurushi vitakavyosafirishwa na ATCL.

Pia amesema mkataba waliyoingia kwa kiasi kikubwa utasaidia kupanua masoko yao hasa hasa kwa yale maeneo yaliyokuwa magumu kufikiwa kwa urahisi.

Amebainisha kuwa baadhi ya majengo ya TPC yatakodishwa na shirika hilo naa kwamba yatapokodishwa itasaidia kulingizia mapato shirika hilo.


Na Abraham Ntambara

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search