Simulizi kali ya SOUDY Brown wa SHILAWADU 'ilivyomkaanga' RC Makonda MCT Report.. #share

REPORI ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) imeweka bayana, jinsi mtangazaji Soudy Brown, wa kipindi cha Shilawadu cha Cloudz, alivyotoa simulizi 'mwanzo mwisho' ya namna Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alivyovamia kituo cha Clouds Media Group (CMG) Machi 17 mwaka huu.


Ripoti hiyo iliyozinduliwa leo jijini Dar es Salaam baada ya kufanyika uchunguzi wa tukio hilo ukiwa na lengo la kubaini kama kitendo hicho kilikuwa na ukiukwaji wa uhuru wa habari.

Itakumbukwa Machi 17 mwaka huu Makonda alidaiwa kuvamia kituo cha CMG akiwa na askari hali iliyopelekewa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye kuunda Tume ili kuchunguza tukio hilo.

Soudy Brown wa Shilawadu ni mmoja wa wafanyakazi wa CMG waliohojiwa na Tume huru ya watu wa nne ikiongozwa na Mwanasheria Juma Thomas iliyoundwa na MCT kuchunguza tukio hilo.

Haya ndiyo maelezo ya Soudy Brown kwenye ripoti hiyo iliyopewa jina la ‘Ripoti ya Uchunguzi wa Uvamizi wa Studio za Clouds TV’ ukurasa wa Tano (5) katika kipengele ‘Ndani ya Studio’.

Brown (mtangazaji wa Shilawadu) aliiambia timu ya uchunguzi kwamba Makonda alipoingia, ilikuwa wakati wa matangazo ya biashara. Aliwauliza kwa nini habari za mwanamke anayedai kuzaa na Askofu Gwajima haijatangazwa.
Brown aliifahamisha Timu kwamba Makonda aliwaambia kama hawangeitangaza, wangepewa mojawapo ya adhabu mbili: kifungo cha miezi sita jela au….(hakutaja adhabu nyingine).

Mtangazaji huyo aliiambia Timu kwamba, alimwelewesha Mkuu wa Mkoa kuwa, Meneja vipindi alimwelekeza aache habari ya mwanamke huyo kwa sababu haikuwa na uwiano kihabari kwa vile Askofu Gwajima ambaye anatuhumiwa hakupatikana kutoa maoni yake.

Kwa mujibu wa Brown, baada ya maelezo yake, Mkuu wa Mkoa alipiga simu kadhaa kabla ya kuondoka kwenye studio, akitishia kuondoka na watangazaji. Dakika chache baadaye Makonda alirejea studioni, safari hii akiambatana na walinzi watatu. 

Akaingia kwenye sehemu ya wahariri akidai apewe ‘kipande’ chenye habari ya ‘yule mwanamke’. Alitoa flash disc(kichoteo), akanakili kilichomo kwenye ‘kipande’ hicho na kuondoka.


Na Mwandishi wetu

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search