TAARIFA MAALUM: Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda kapokea ugeni kutoka Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM) walipofika shambani kwake.. #share

P.O Box 70089; Dar es Salaam
NSSF-MAFAO House. 15th flr Uhuru Road, Ilala Boma
Tel: +255 732 975 799
Email: toam@kilimohai.org
Website: www.kilimohai.org
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI Mkuu Mstaafu wa awamu ya nne Mh. Mizengo Pinda amesifu jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Uendelezaji Kilimo Hai Tanzania (TOAM), kwa kile alichokiita kuwa jitihada za uendelezaji kilimo haikwa sasa ni jambo lisiloepukika.
Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Mizengo Pinda, akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM) baada ya mazungumzo kuhusu kilimohai shambani kwake Zuzu Mkoani Dodoma |
Mh. Pinda ameyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma baada ya kutembelewa nyumbani kwake Zuzu na Mkurugenzi Mkuu wa TOAM nchini ambaye pia ni Rais wa Mtandao wa Kilimo Hai Barani Afrkika, Bw. Jordan Gama.
Nakushukuru ndugu Gama kwa kunitembelea hapa kijijini kwetu , mimi nimeweka makazi hapa, na hakika naendesha kilimo kwa asilimia kubwa kufuata mfumo wa kilimo hai, nafanya hivi kwasababu naelewa umuhimu wa kupata chakula salama lakini vile vile umuhimu wa kuilinda ardhi na viumbe vilivyomo ndani yake.
Niliamua tangu awali kujikita katika kilimo cha namna hii, na kwa kweli ninakifurahia, kwa kuwa natumia mbolea ya samadi itokanayo na wanyama ninaowakuza hapa hapa shambani, lakini kabla nilikuwa Napata kwa wafugaji ambao baadaye walianza kuuza kwa gharama ya TZS 35,000 kwa lori, lakini kubwa zaidi ni kwamba uzalishaji kwa kutumia mbolea ya samadi hufanya mazao yahimili hali ya ukame na kupata mavuno kuliko mazao ya shamba lisilotumia mbolea hii, alisema Waziri Mkuu Mstaafu.
Mh. Pinda ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa umma na viongozi mbalimbali nchini na dunia kwa ujumla kujenga utamaduni wa kujiwekeza kwenye kilimo, kwa kuwa kilimo kimekuwa na tabia ya kumlinda na kumsitiri yeyote yule mwenye malengo ya kuishi maisha ya kipato cha kati na hata ya kiwango cha juu baada ya kustaafu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TOAM, Bw. Gama, alimwambia Waziri Mkuu Mstaafu kuwa amevutiwa kufanya ziara katika shamba hilo baada ya kuona jitihada zake kubwa katika kujaribu kulima kwa mfumo wa kilimo hai kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Mh. Waziri Mkuu mstaafu, nichukue fursa hii kukupongeza kwa uamuzi wako wa kuwa mfano mwema kwa wastaafu na watanzania kwa ujumla, sisi TOAM, tutashirikiana nawe bega kwa bega katika kuhamasisha na kuelimisha jamii kuiga kilimo cha aina hii unachokiendesha,bila shaka ziara hii hapa leo itafungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika jitihada zako za kuendeleza kilimo endelevu.
Tumejionea bayana kuwa eneo hili ni kame sana, na kwamba baadhi ya mazao pamoja na jitihada zako za kufanya umwagiliaji yanaweza yasifanye vyema sana, tunaomba uturuhusu tulete mimea itakayosaidia kuongeza rutuba na kutunza unyevu katika ardhi ili mazao yaweze kukua vema, kupitia kazi yako hii ya kilimo tunaona fursa kwetu ya kufanya shamba hili kuwa kitivo cha mafunzo kwa wakulima wa kada zote.
Gama akaongeza kuwa kwa sasa sehemu kubwa ya dunia mwamko wa kilimo kwa mfumo wa kilimo hai umekuwa mkubwa sana, na kwamba nchi za ulaya zenye uchumi mkubwa kama Ujerumani kasi ya kubadili mashamba yao kutoka kilimo cha kutumia kemikali inaongezeka na kuwa ya kilimohai, lakini kubwa zaidi ni kwamba katika nchi hiyo kilimo cha kutumia pembejeo zilizobadilishwa vinasaba (GMO) hakijaruhusiwa na mamlaka zote za kiserikali.
Akizungumzia kuhusu GMO, Mh. Pinda alisema serikali wakati akiwa madarakani iliruhusu utafiti wa GMO ili kujiridhisha pasipo shaka kuhusu usalama na manufaa ya teknolojia hiyokwani imekuwa na mtazamo uliogawanyika kote duniani na nchi mbalimbali kuchukua maamuzi ya kuiruhusu au kuizuia ili kujiridhisha na hoja zinazokinzana.
Wakati huo huo, barani Afrika, nchi ya Ethiopia imetajwa kuwa ni mojawapo ya nchi inayopiga hatua kwa kasi zaidi kwa ongezeko la wazalishaji wa bidhaa za kilimo hai ikifuatiwa na Tanzania.
Miongoni mwa majukumu ya TOAM ni kuwaunganisha wakulima na masoko, ili kuongeza tija kwa katika uzalishaji, miongoni mwa taasisi zinazozalisha kwa mfumo wa kilimo hai nchini ni pamoja na Vyama vya Ushirirka vya Kagera (KCU); Kilimanjaro (KNCU) na kampuni binafsi (BIORE) zinazofanya biashara na uzalishaji wa bidhaa/mazao kwa kuzingatia viwango na mfumo wa kilimohai.
Taasisi ya uendelezaji kilimo hai nchini yaani Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM), ni taasisi mwamvuli, ambayo inaunganisha wadau mbalimbali wa kilimo hai, wakiwemo, wazalishaji, watafifiti na waelimishaji, wauzaji, makampuni na asasi za kiraia pamoja na vikundi vinavyozalisha mazao kwa mfumo wa kilimo hai.
Kwa sasa makao makuu ya kilimo hai barani Afrika yapo nchini Tanzania, na Rais wa Kilimo Hai ni Mtanzania, na kwamba taasisi hii inafanya kazi kwa karibu sana na serikali kupitia Wizara ya Kilimo, sambamba na mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na kilimo hai kama International Forum for Organic Agriculture Movement (IFOAM), United Nation Conference on Trade and Development (UNCTD) na African Union Commission (AUC).
Imetolewa na:
Constantine Akitanda
Mshauri wa Mawasiliano
Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM)
No comments:
Post a Comment