uCHAGUZI kENYA: Mbeki aupa tano, aipongeza Serikali na Tume ya Uchaguzi IEBC...#share

NAIROBI- KIONGOZI wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika (AU), Thabo Mbeki, amesema shughuli ya upigaji kura nchini ilikuwa ya uwazi na wameridhishwa huku matokeo ya awali hadi jana jioni yakionesha kuwa Rais Uhuru Kenyatta anaongoza kwa kura 8,096,122 dhidi ya 6,695,221 za mpinzani wake, Raila Odinga

Licha ya upigaji kura kuwaridhisha, Mbeki alisema kulikuwa na changamoto kadhaa kama vile, kufanana kwa ukaribu zaidi kwa rangi mbili za karatasi ziliyokuwa zikitumika kupigia kura lakini tatizo hilo lilitatuliwa na maofisa wa tume kwa kuwasaidia raia kutofautisha rangi hizo..

Kiongozi huyo ambaye ni rais wa zamani wa Afrika Kusini, ameipongeza Serikali na Tume ya Uchaguzi na Mipaka Kenya (IEBC) kwa kuhakikisha wafungwa wamepiga kura. Idadi ya wapigakura nchini humo ni milioni 19.6.

“Tunafahamu kwamba IEBC bado inahesabu na kukagua matokeo. Shughuli ya uchaguzi bado inaendelea, hivyo bado ni mapema,”  alisema Mbeki na kuongeza;

“Hata hivyo, waangalizi wa AU wanafurahi kwamba uchaguzi ulikuwa wa amani, siku ya uchaguzi watu walifika kwa wingi, na waliruhusiwa kupiga kura kwa kufuata taratibu za uchaguzi Kenya na zinazokubaliwa na AU,” alisema Mbeki.

Aidha, Mbeki aliongeza kuwa waangalizi hao wanaweza kusema kusema shughuli walizohesabu, upigaji kura na upeperushaji wa matokeo, vilitimiza viwango vya ubora vya Kenya na AU.

Alisema wamepokea malalamiko kuhusu upeperushaji wa matokeo na kutoa mwito kwa wadau kutumia mifumo wa kisheria iliyopo.
Mbeki alisema maofisa wa juu kutoka Muungano wa Upinzani nchini (NASA), walikutana na waangalizi wa AU na kuwapa ripoti kuhusu madai ya udukuzi wa mitambo ya IEBC.

Mara baada ya maofisa hao kuwasilisha madai hayo, Mbeki alieleza kuwa waliamua kuwahoji kuwa walipata vipi nyaraka hizo walizokuwa nazo za madai ya udukuzi.

“Maofisa hao wa NASA walijibu kuwa, walipewa ‘ufunguo’ fulani na IEBC wa kuweza kuingia kwenye seva. Hata hivyo, tuliwaambia kwamba, kwa kufuata fomu 34A itawezekana kwa kila mtu kubaini matokeo halisi,” alisema Mbeki.
Upinzani ulitilia shaka uhalisia wa fomu hizo na kusema katika baadhi ya vituo vya kupigia kura hawakuwa na maajenti na katika baadhi, maajenti wao walizuiwa kuingia.

Aidha, upinzani ulisema huenda fomu 34A katika baadhi ya vituo zilifanyiwa mabadiliko.

Kwa upande mwingine, Mbeki alibainisha kuwa wao kama waangalizi wa AU hawawezi kuzungumzia madai ya upinzani kwamba mitambo ya IEBC ilidukuliwa na kuongeza kuwa jukumu lao ni kuangalia shughuli ya uchaguzi inavyofanyika.

“Sisi si wachunguzi wa uchaguzi. Iwapo tungeona kitu kikifanywa vibaya, kinyume na sheria za Kenya na viwango vya AU, basi hapo tungeingilia kati,”
“Katika baadhi ya visa, NASA wamewasilisha malalamiko kwetu kuhusu uchaguzi, mfano kupatikana kwa usajili wa wapiga kura na usalama na kusafirishwa kwa maofisa takriban 40 wa polisi kwenda kwingine,”

“Tuliangazia hayo, na baadhi tukawapasha IEBC kuhusu malalamisho ya usajili na kuhusu polisi tukawasiliana na kukutana na Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang'I,” alisema Mbeki.


Naye mjumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Madola, Rais wa zamani wa Ghana, John Dramani Mahama alisema walikutana na Odinga na wajumbe wake na walitoa madai ya kompyuta za IEBC kuvamia huku wakiwa na nyaraka kama ushahidi wa madai yao, hata hivyo Mahama alisema nao waliwaeleza kwanza hawana utaalamu wa teknolojia hiyo, lakini jukumu lao ni kuangalia kama utaratibu mzima wa uchaguzi umefuata sharia na katiba ya nchi na madai mengine ya ukiukwaji wa taratibu yana utaratibu wake uliowekwa kwa mujibu wa sharia.

Na Mwandishi Wetu

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search