gOOD nEWS: Serikali Kuanzisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi...Lengo kuwezesha Wataalamu wa...#share
SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano inatarajia kuanzisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) ili
kuzalisha wataalamu wa ngazi ya kati wenye ubobezi katika sekta ya ujenzi.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Barabara, John Ngowi kwenye kongamano la pili la kujadili hatua zilizofikiwa
juu ya uanzishwaji wa Taasisi hiyo.
Ngowi alisema kuwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo nchini
kutaondoa pengo la uwiano baina ya wahandisi na kada za chini kama mafundi
sanifu na mafundi mchundo ambao ndio wasimamizi wa karibu wakati kazi za ujenzi
zinapotekelezwa.
“Mpango mkakati wa Wizara yetu pamoja na mambo
mengine, unahusisha uimarishwaji wa sera zinazohusu ujenzi kwa kujenga mazingira
wezeshi, mafunzo ya ufundi na matumizi ya teknolojia, mkakati ambao utawezesha
kutatua changamoto za umahiri na ubobezi inayokabili sekta ya ujenzi,” alisisitiza
Ngowi.
Aidha, Ngowi aliongeza kuwa uanzishwaji wa taasisi
hiyo itakuwa chachu ya kufikia azma ya Serikali kuelekea uchumi wa kati wa
viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kuongeza rasilimali watu ambao ni muhimu katika
usanifu, usimamizi, ujenzi na ukarabati wa miundombinu.
Mwenyekiti wa kampuni ya EcomResearch ambayo ni mshauri
wa uanzishwaji wa ICoT, Profesa Godwin Mjema alisema mipango ya uanzishwaji wake uko katika hatua nzuri na
umeshirikisha wadau ili kujadili kozi na mitaala itakayotumika kufundishia.
“Sisi kazi yetu ni kushauri na leo tumekutana na
wadau kujadili hatua tuliyofikia, wadau watajadili na kukubaliana na tuliyoandaa,
wakikubaliana nasi tutakabidhi kwa Wizara ambao ndio wamiliki na wao
watawasilisha Baraza la Taifa Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa hatua za usajili,”
alisema Profesa Mjema.
Kuanzishwa kwa taasisi hii kunatokana na kuongezeka
pengo kati ya wahandisi na kada za chini hali iliyotokana na vyuo vingi vya
ufundi kupandishwa hadhi kuwa vyuo vikuu katika miaka ya 1990 bila kuanzishwa
vyuo vingine vya ngazi ya kati hasa vya ujenzi.
Na Mwandishi Wetu



No comments:
Post a Comment