Japani yaipatia Tanzania sh. trioni 1.4 kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo--Dar es Salaam.....#share

Dar es Salaam, Septemba 1, 2017:
Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), imeipatia Tanzania
ruzuku ya Yen milioni 69 sawa na Shilingi trioni 1.4 kwa ajili ya kufanya
usanifu wa kina wa awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa barabara ya New
Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo yametiwa
saini leo Septemba 1, 2017, Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kwa niaba ya Serikali, Balozi wa Japan
nchini Tanzania Masaharu Yoshida na Mwakilishi Mkazi Mkuu wa Shirika la
Maendeleo la Japani (JICA), Satoru Matsuyama.
Tukio hilo limekwenda sambamba na
kuingia makubaliano kuhusu muda wa kukamilisha mradi huo pamoja na kupeana
taarifa ya namna mradi huo utakavyotekelezwa.
Mradi wa barabara hiyo yenye urefu
wa kilometa 4.3 utahusisha barabara yenye njia nne pamoja na kuanza kwa awamu
ya nne ya barabara itakayotumiwa na mabasi ya mwendo wa haraka (BRT phase IV).
Akizungumza baada ya kutiwa saini ya makubaliano hayo, Dkt. Mpango amesema kuwa barabara hiyo ikikamilika
itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya msongamano wa magari kutoka
na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Ameishukuru Japan kwa msaada huo wa
awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo katika awamu ya kwanza, Japan
ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 99.5. kujenga barabara ya njia nne katika kipande
cha kilometa 12.9 kutoka makutano ya barabara ya Tegeta na makutano ya barabara
ya Mwenge.
“Si mara ya kwanza kwa Japan
kuisaidia Tanzania, wanajenga barabara za juu katika makutano ya Tazara, ujenzi
wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Dodoma hadi Babati mkoani Manyara (km
188.15), Tunduru-Mangaka – Mtambaswala (km 202) na barabara ya Iringa hadi
Dodoma (259.9)” alisisitiza Dkt. Mpango.
Amesema kuwa upanuzi wa barabara ya
Bagamoyo si tu kwamba itapunguza msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam lakini
pia utaunganisha Jiji na Bandari ya Bagamoyo ambayo ni muhimu kwa ajili ya
usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma kutoka Jijini, mikoa ya Pwani na maeneo
mengine ya nchi.
Balozi wa Japan, Mhe. Masaharu
Yoshida ameeleza kuwa kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa awamu ya pili ya
barabara ya Morocco hadi Mwenge kumekuja baada ya kukamilika kwa awamu ya
kwanza iliyohusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Tegeta hadi Mwenge
ili matokeo ya mradi huo yaweze kuonekana dhahiri.
Ameahidi kuwa baada ya kukamilika
kwa usanifu wa kina wa barabara hiyo, Serikali ya Japan kupitia JICA, itasaini
mkataba wa kuanza ujenzi huo Mwezi Juni mwakani.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu
Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Satoru Matsuyama, amesema
Japan imeamua kufadhili mradi huo baada ya utafiti kuonesha kuwa Barabara ya
Bagamoyo ndiyo yenye msongamano mkubwa wa magari ambapo inakadiriwa kuwa magari
52,000 yanapita kila siku katika barabara hiyo.
Ameelezea matumaini yake kwamba
mradi huo utakapo kamilika utasaidi kukuza shughuli za kiuchumi katika Jiji la
Dar es Salaam kwa kuwa ndicho kitovu cha biashara kwa maeneo mengine ya
ndani ya nchi na kimataifa na kuwaomba wataalamu pamoja na TANROADS kuharakisha
usanifu huo wa kina.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Barabara Nchini-TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa ujenzi wa
barabara hiyo hautahusisha ubomoaji wowote wa makazi ya watu wala majengo ya
biashara.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipan
No comments:
Post a Comment