Madereva 7 Wa Mabasi ya Abiria Wafutiwa Leseni...Soma Habari Kamili na Matukio360 Kujua Sababu..#share
Jeshi la Polisi-Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania limewakamata madereva saba wa mabasi ya abiria na kuwafutia leseni za udereva baada ya kukamatwa wakiwa wanaendesha mwenddo kasi hatarishi wa zaidi wa kilomita 90 kwa saa.

Aidha, kikosi hicho kwa kushirikiana Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini nchini (Sumatra) kimeyafungia mabasi 11 ya kampuni mbalimbali kutoa huduma ya kusafirisha abiria kwa makosa ya mwendokasi mpaka yatapohakikiisha vifaa vya kudhibiti mwendo huo vilivyofungwa katika mabasi hayo vinafanya kazi ipasavyo.
Hayo yamesemwa leo na Kamnda wa kikosi hicho nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi(SACP), Fortunatus Musilimu wakati akizungumza na wanahabari kuhusiana na oparesheni ya mchana na usiku inayoendelea ya kukamata madereva wa mabasi wanaokiuka sheria za barabarani.
Amesema katika oparesheni hiyo inayofanyika usiku na mchana madereva hao walikamatwa sehemu tofauti wakivunja sheria ya mwendokasi huku akisisitiza kutokana mamlaka aliyopewa amefuta madaraja C na E katika leseni zao ambapo hawataruhusiwa kuendesha magari ya abiria na mizigo kwa kipindi cha miezi sita mpaka watakaprudi darasani na kwamba watakapotahiniwa ndipo watarejeshewa madaraja yao.
" Kwa mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa Sheria ya Usalama barabarni, Tangazo la Serikali na. 31 la mwaka 2015, kanuni na 5 ya sheria hiyo, nafuta madaraja C na E katika leseni za madereva hao hivyo hawaruhusiwi katika kipindi cha miezi sita kuendesha magari ya mizigo na abiria hadi wakasome darasani watahiniwe tena mpaka wafaulu ndipo warejeshewa madaraja," alisema Kamanda Musilimu.
Aliwataja madereva hao ni Hamad Salum, Kija Mayenga, Isack Mbijina, Hassan Semazua, Stanley Mosha, Abdallah Hussein na Sempunda Yusuf.
Amessisitiza kuwa madereva walipofikishwa mahakamani walikiri makosa na kutozwa faini ya sh 100.000 hadi sh 300,000.
Ameongeza kuwa kikosi hicho kimewafutia leseni za udereva madereva walioasababisha ajali na vifo hivi karibuni akiwemo Ismail Nyami aliyesababisha ajali Septemba 23 mwaka huu iliyoua watu wawili na kujeruhi 42 wilayani Nyasa, Mkoani Ruvuma pamoja na dereva Mseka Salum aliyesababisha ajali Septemba 25 iliyoua mtu mmoja na kujeruhi wengine 25 katika eneo la Maganzo wilayani Kishapu, Shinyanga pamoja na Malick Hassan aliyesababisha ajali ya kugonga Ng'ombe usiku na kupinduka Septemba 21 mwaka huu ambapo mtu mmoja alipoteza maisha na sita kujeruhiwa.
Amefafanua kuwa madereva wote waliofungiwa leseni tayari taarifa zimeshafikishwa kwa waajiri wao, Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (Taboa),Mamalaka ya Mapato na Sumatra.
Aidha, amesema katika kipindi cha wiki moja kuanzia Septemba 18 hadi 24 tangu kuanza kwa oparesheni hiyo jamla ya makosa 53,870 ya magari yamekamatwa na kwamba idadi hiyo ya wiki moja kabla kuanzia Septemba 11 hadi 17 ni makosa 53,053 hivyo inaonyesha kuwepo kwa ongezeko la makosa 817 yaliyokamatwa.
Ameongeza kuwa oparesheni hiyo imeleta mafanikio kwa kupungua kwa ajali, vifo na majeruhi na kubainisha kuwa mwezi Septemba 18 hadi 24 ajali zilikuwa 37, vifo 26 na majeruhi 54 ukilinganisha na takwimu hizo kwa kipindi hicho kuanzia Septemba 11 hadi 17 jumla ya ajali 66, vifo 42 na majeruhi 107 zinaonyesha kuwepo upungufu wa ajali 29 ambazo ni sawa na asilimia 44, upungufu wa vifo 16 ambavyo ni sawa na asilimia 38 na upungufu wa majeruhi 53 sawa na asilimia 50.
Amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa askari ili kudhibiti ajali za barabarani na kuwataka madereva kutii sheria hizo kwani makosa hatarishi hayatakuwa hayatozwa faini badala yake watakamatwa na kuwekwa mahabusu, kuelekwa mahakamani kisha kufungiwa leseni zao.
Na Hussein Ndubikile
No comments:
Post a Comment