Mwigulu Nchemba: Tunasubiri Tundu Lissu Apone..Soma Habari Kamili na Matukio360..#share

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema   uchunguzi wa tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Tundu Lissu anaamini utafanikiwa akipona. kwani anategemewa kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha upelelezi wa tukio hilo.
Image result for mwigulu nchemba
Akizungmza leo na kituo cha televisheni cha Clouds amesema wanamuombea Lissu apone kwani ni matarajio yao kwamba akipona atatoa  mchango mkubwa wa kusaidia uchunguzi kwani kwa sasa kutokana na kuwa na maumivu makali hawezi kuulizwa chochote. 

Amesema kutokana na upya wa uhalifu wa kushambulia watu kwa risasi kama ilivyotokea kwa Lissu, kuna mambo ambayo wanaendelea kuyafuatilia ili kubaini kiini cha uhalifu huo.

“Suala la Lissu kutokana na upya wake, kuna vitu tunaendelea kuvifuatilia, hivyo kuna mambo hatuwezi kuyasemea,” amesema.

Amewataka Watanzania waendelee kuwa na subira kwa kuwa kazi inaendelea kufanyika.

Mwigulu amesema baada ya tukio la kushambuliwa Lissu Septemba 7, taarifa kadhaa zilichukuliwa eneo la tukio ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ili kupata undani wake.

“Wahalifu hawajakamatwa wote, ukianza kusema itakuwa ni shida, kuna mambo yanaendelea kufanywa na hayana ukomo. Ukomo utafikiwa endapo wote waliohusika watakamatwa. Nikisema naweza kuvuruga kazi inayoendelea,” amesema.

Akijibu swali la mtangazaji wa kipindi hicho kuwa watu wanahoji kwamba askari wanapouawa wahalifu wanakamatwa mapema Mwigulu amesema, “ Watu wakiwaza hivyo watakuwa wanakosea, hatuweki madaraja, ni mazingira ya tukio tu.”

Akizungumzia uchunguzi unaoendelea kuhusu kuvamiwa kwa Lissu amesema hawezi kueleza waliokamatwa bali tayari kuna magari zaidi ya 10 yanayofanana na lililohusika kwenye tukio yamekamatwa.

Mwigulu amesema alimuona Lissu siku ya tukio Septemba 7 akiwa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma na baadaye uwanja wa ndege aliposafirishwa kwa ajili ya matibabu jijini Nairobi nchini Kenya ambako yuko hivi sasa.

Amesema hajafika Nairobi kumjulia hali Lissu bali kwa Mkoa wa Singida, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amefika.

“Katika mazingira mengine tunaendelea kupata taarifa, kama Serikali tuna balozi,  kama waziri kwenda kumuona ni jambo jema katika utaratibu wa uchunguzi hata dereva tutazungumza naye,” amesema.

Amesema dereva hivi sasa anapata tiba ya kisaikolojia na anaamini atakapokuwa tayari atazungumza na wanaokusanya taarifa.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search