Ni Rasmi sasa Wakimbizi wa Burundi nchini kuanza kurejea kwao Septemba 7 mwaka huu....#share
WAKIMBIZI wa Burundi waliokimbia
machafuko nchini kwao wataanza kurejea nchini kwao ifikapo Septemba 7 hadi
Desemba 31, mwaka huu mara baada ya pande tatu ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani
(UNHCR), kutiliana saini Mpango wa Kuwarejesha wakimbizi baada ya mkutano
uliochukua takribani siku tatu katika kuandaa mpango huo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwigulu Nchemba,akibadilishana nyaraka na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia
Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya(kulia) zenye
makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa
mkoani Kigoma. Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki, Ukumbi wa
Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Picha na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Wakitiliana saini makubaliano hayo
yaliyofanyika mwishoni mwa wiki,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu
Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi,
Pascal Barandagiye na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani
(UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya, mwishoni mwa wiki wote walikubaliana
kutekeleza vipengele vilivyopo katika makubaliano hayo yakiwa na lengo la
kuwarudisha wakimbizi walioomba kurejea nchini Burundi, baada ya hali ya Amani
na utulivu kurejea.
Akizungumza baada ya kutiliana
saini makubaliano hayo Waziri Mwigulu, alisema umefika wakati wa
wakimbizi wa Burundi kurudi nchini kwao kuungana na familia zao na ndugu
waliobaki ili kusaidia kujenga uchumi wa nchi yao baada ya kuwa katika
machafuko yaliyosababisha kukimbia nchi yao kwa muda mrefu.
“Mimi kama mwanauchumi ninaona
madai yao ya kurudi nchini Burundi kujishughulisha na shughuli za kilimo ni
maamuzi mazuri huku pia wakisisitiza kurejea kwa Amani na Utulivu nchini kwao
kuwa ni sababu ya msingi ya kufikia kuomba kurejea, sisi kama Serikali
tutahakikisha zoezi hilo la urejeaji nchini kwao linaenda salama tukishirikiana
na Serikali ya Burundi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchini Burundi,”
alisema Mwigulu.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu
ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, akibadilishana nyaraka
na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini
Tanzania, Chansa Kapaya (kulia) zenye makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha
Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Katikati ni Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa
wiki, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Picha
na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani na
Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, amesema
anaishukuru Serikali ya Tanzania na Watanzania wanaoishi kwenye maeneo
yaliyotumika kuwahifadhi wakimbizi kwa ukarimu wao walioonyesha muda wote kwa
raia kutoka nchini Burundi huku akisisitiza kurejea kwa hali ya Amani na
utulivu ambao hapo mwanzoni ilitoweka.
“Nawaomba wananchi wetu warejee
nchini ili tuweze kuijenga Burundi yetu ambayo hivi sasa kuna Amani na utulivu,
pia naishukuru Serikali ya Tanzania na Watanzania ambao wamekua wakiwaonyesha
ukarimu wakimbizi kutoka Burundi na kuwapa hifadhi nchini
hapa,”alisema Barandagiye.
Kwa upande wao Shirika la Kuhudumia
Wakimbizi Duniani (UNHCR) kupitia kwa Mwakilishi wao nchini, Chansa
Kapaya, wameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha wakimbizi wa
Burundi 6,800 walioomba kurejea nchini kwao wanasahiliwa na kurejeshwa kwao
katika hali ya utu na usalama huku shirika hilo likizishukuru Serikali za
Tanzania na Burundi kwa msaada wao walioupata katika kushughulikia masuala ya
wakimbizi.
Na Mwandishi Wetu
No comments:
Post a Comment