UVCCM waungana na Mbowe kupigwa risasi kwa Lissu ... Waijibu BAVICHA kwa kudai Lissu si wa kwanza...#share.

*TAARIFA  YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWA VYOMBO VYA HABARI  ILIYOTOLEWA NA  KAIMU KATIBU MKUU WA UVCCM SHAKA HAMDU SHAKA (MNEC) UPANGA DAR ES SAALAM  SEPTEMBA, 10  2017 UPANGA JIJINI DAR ES SALAAM *

Ndugu Waandishi wa Habari

Septemba 9 Mwaka huu Baraza la Vijana Chadema(BAVICHA) kupitia Mwenyekiti na Katibu Mkuu  wake walikutana na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kutoa matamshi ya kebehi, yanayojenga utata na mkanganyiko.

Matamshi ya BAVICHA yana nia na lengo la kupalilia chuki na hasama kwani yamethubutu kuingilia medani za kintelejinsia na upelelezi kufuatia tukio la kusikitisha la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki Mheshimiwa Tundu Antipius Lissu na watu wasiojulikana.

Sehemu kubwa katika maelezo ya Viongozi hao kwa nyakati tofauti hayakuonyesha ukomavu, busara wala  hekima ukilinganisha na ukubwa wa tatizo la kushambuliwa kwa Mheshimiwa Lissu huku wakidhani jambo hilo limewafurahisha watanzania ila linawauma mno BAVICHA kuliko wananchi wengine.

Fikra na mtazamo huu wa BAVICHA licha ya kutakiwa kulaaniwa vikali na kila mmoja wetu pia  yana nia potofu ya kutaka kuiyumbisha  jamii hivyo yasipewe nafasi kwani yanapaswa kupuuzwa na watanzania wote werevu, wapenda amani, umoja na mshikamano.

Kitendo cha Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake  kuishutumu Serikali na na kudai eti inaendeshwa kwa mfumo kandamizi si tu kama ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu  lakini pia ni matamshi yaliokosa staha yakitolewa wakati huu.

Tukio la kushambuliwa Mheshimiwa Tundu Lissu na watu wasiojulikana si jambo dogo na jepesi kama inavyochukuliwa na BAVICHA na viongozi wake ambao wameshindwa kupima uzito wa maneno yao kabla kutamka  na thamani kamili ya amani, heshima na utulivu uliopo nchini mwetu.

Ndugu waandishi wa Habari

Yapo matukio mengi ya kijambazi huko nyuma yamewahi kutokea. Mengine yamepoteza maisha ya viongozi wa juu wa Serikali na kukatisha  maisha yao kabla ya tukio hili la Mheshimiwa Lissu.

Amepigwa risasi nane kifuani Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Sheikh Abeid Amani Karume akapoteza maisha, pia ameuwa aliyekuwa Waziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Nickas Mahinda Mkoani Morogoro  kwa tukio la  kupigwa risasi .

Matukio ya ujambazi yanayofanywa na watu wasiojulikana   kupiga watu risasi ni mambo yanayotokea hata katika Mataifa makubwa na baadhi ya matukio mara nyingi  upelelezi wake huchukua miaka na muda mrefu hadi wahusika kutambuliwa au kukamatwa.
Marekani marais wawili katika familia moja  ya kina F. Kennedy wameuawa katika mazingira ya kihalifu  lakini pia Rais Anuar Saadat wa Misri aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa anakagua gwaride.

Umoja wa Vijana wa CCM unawakanya Bavicha nakuwataka waache kiherehere cha kuingilia taratibu za kiutawala na upelekezi, yanapotokea masuala mazito yakihusisha maisha ya watu, kushambuliwa au kutekwa na wao  kutaka kuyageuza yaonekane katika muktadha wa kisiasa.

BAVICHA wamejitahidi kuanisha matukio kadhaa walioyaita yamefanywa na watu wasiojulikana, upelelezi wake kutojulikana na kutaja baadhi ya majina ya watu  waliokumbwa na kadhia ya matukio hayo huku wakikwepa kutaja hata mfululizo wa mauaji ya viongozi wa CCM na Serikali huko Kibiti Mkoani Pwani.  Vile vile BAVICHA wamekwepa kutaja kiini cha kifo cha kushangaza cha Marehemu  Chacha Zakayo Wangwe.

Ndugu Waandishi wa Habari.

UVCCM kwa mara ya kwanza tunaunga mkono matamshi yaliotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Ndugu Freeman Aikael Mbowe aliposema "huu si wakati wa kunyooshena vidole vya lawama na shutuma huku akivitaka vyombo vya Usalama vitimize wajibu wao kiufundi na kitaaluma".

Mbowe ametamka matamshi yaliopevuka kifikra, kiupeo  na kisiasa tofauti na povu lilivyowatoka vijana wake na kuonyesha uchanga katika siasa huku wakilitumia tukio hili la huzuni la  kushambuliwa Mheshimiwa Lissu liwe jukwaa lao la kufanya siasa.

Kwanini BAVICHA katika maelezo yao hawakugusia wala kuhoji ni kina nani waliomuwekea sumu Dk Harrison Mwakyembe mpaka akadhurika na kutoka unga  mwilini. Je, BAVICHA tayari wana majawabu ni nani aliyehusika kumpa sumu Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kule Bagamoyo?.

UVCCM tulitegemea kuona huo ujasiri wao wanaojigamba na kuwapa kiburi cha kuhoji, wangehoji mazingira tata ya kifo cha Profesa Kighoma Ali Malima Uingereza  au  kifo cha Kapteni Ditopile Ukiwaona Mzuzuri Mkoani Morogoro .

Kwa kutanguliza mbele maslahi ya umma, kujali na kuendelea kudumisha misingi ya Amani, Umoja wa kitaifa na Mshikamano wetu. Wote  tukiwa ni watanzania  tuvipe nafasi na muda vyombo vya usalama kuchunguza kwa undani na umakini suala hili na kulitolea maelezo.

Umoja wa Vijana wa CCM tunaendelea kushauri ni vema kwa wakati huu tukaongozwa na busara kuliko pupa na ushabiki ambao unaweza kuliingiza taifa katika machafuko yasiyo na msingi na kuharibu tunu ya taifa letu ya Amani, Umoja na Mshikamano.

Vile vile tunatumia nafasi hii kumuomba Mwenyezi Mungu amponyeshe haraka Mhe. Tundu Antipus Lisu ili aje kushirikiana na Watanzania wenzake kujenga na kuliendeleza taifa letu.

*KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
*

Imetolewa na;
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU UVCCM TAIFA

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search