CCM: Serikali hakikisheni pembejeo za kilimo zinaviwango...Soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi ameishauri serikali kuhakikisha Pembejeo za kilimo wanazouziwa wakulima zinakuwa na viwango vinavyoendana na mazingira ya kilimo yaliyopo nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Mabodi akiwahutubia wakulima na wananchi katika uzinduzi wa kilimo cha mpunga bonde la mahekani Kizimbani Unguja.

Ushauri huo ameutoa leo wakati akizindua msimu wa kilimo cha Mpunga katika mabonde yaliyopo katika Jimbo la Bububu na vitongozi vyake uko katika bonde la Mahakani lililopo katika kijiji cha Kizimbani Wilaya ya magharibi "A" .


Amesema wananchi wengi wanafanya shughuli za kilimo katika mazingira magumu hivyo ni lazima taasisi za umma zinazohusika na kuuza pembejeo za kilimo ambazo ni mbolea, dawa na mbegu kuwa makini kwa kuhakikisha
bidhaa hizo zinakidhi vigezo vya kilimo ili kuepusha hasara kwa wakulima.


Dkt. Mabodi ametoa ufafanuzi huo baada ya Mwakilishi wa jimbo la Bububu, Mh. Masoud Abrahman Masoud kueleza kuwa katika msimu wa kilimo ulipita baadhi ya wakulima wanaolima mpunga katika mabonde ya mpunga ya jimbo hilo walipata walikosa mavuno kutokana na mpunga kukauka kwa sababu ya kutumia pembejeo mbovu zisizokuwa na viwango.



"Nitakaa na viongozi wa Wizara husika kwa lengo la kuwaeleza changamoto hiyo nao waweze kuifanyia kazi ili isiweze kujitokeza katika misimu ijayo.", alifafanua Dk. Mabodi na kuwasihi wakulima wasivunjike moyo kwani serikali yao ni makini na ina dhamira ya kuhakikisha ardhi ndogo iliyopo inatumika kwa kilimo cha kisasa.


Ameeleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 imeahidi 
kuisimamia serikali kuhakikisha inaweka miondombinu endelevu ya kilimo itakayosaidia Zanzibar kulima mazao ya aina mbali mbali hasa mpunga kwa lengo la kupunguza uagizishiaji wa chakula kutoka nje ya nchi.

Amesisitiza wakulima hao kuhakikisha wanaendelea kufanya maandalizi 
mapema ya msimu wa kilimo cha mpunga na mazao mengine ili kwenda sambamba na msimu wa mvua kwa lengo la kupata mavuno mengi.


Hata hivyo amewasihi kuwatumia wataalamu wa kilimo ili waweze kutoa ushauri wao juu ya mbegu zinazostahili kupandwa kwa mujibu wa maeneo husika ya kilimo.



Amewapongeza viongozi wa Jimbo la Bububu ambao ni Mbunge, Mwakilishi na Madiwani kwa ushirikiano wao unaozaa matunda ya kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020  kwa vitendo kwa kuanzisha mradi wa kilimo cha mpunga unaowanufaisha wakulima wengi wa jimbo hilo.


Akizungumzia uchaguzi unaondelea ndani ya CCM Dk.Mabodi amesema msimamo wa chama hicho ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa wanakuwa ni viongozi safi kimatendo, kimaadili na wanaokubalika katika jamii na wenye uwezo wa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa dola wa  mwaka 2020.


" Ajenda ya wapinzani ni kuzungumzia uchaguzi uliopita na kuzua na kuaminishana mambo ambayo hayawezekani kutekelezeka lakini CCM kazi yetu kubwa ni kuwapelekea maendeleo wanachama wetu popote walipo nasi

tunawafikia", alisema Dk. Mabodi.



Sambamba na hayo Dk.Mabodi ameahidi kuchangia nusu ya fedha za kununua tirekta ndogo aina ya powertiller ili iweze kuwasaidia wakulima hao katika shughuli za kilimo.



Naye Mbunge wa Jimbo hilo,  Mwantakaje Haji Juma amesema mradi huo wa kilimo cha mpunga umeendeshwa kwa awamu tatu na kuwapatia wananchi mafanikio makubwa ya chakula na awamu ya sasa jumla ya shilingi milioni 16 zinatarajia kutumika fedha zitakazotolewa na mbunge na
mwakilishi wa jimbo hilo.



Akisoma risala kwa niaba ya wakulima wa jimbo hilo, Bw. Saleh Said Njonjo amezitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na kupunguziwa bei ya pembejeo za kilimo pamoja na kupunguziwa bei ya kulimiwa na matrekita ya serikali katika mabonde yao.



Hata hivyo amesema kuwa jumla ya wakulima 723 wa jimbo hilo na maeneo jirani watanufaika na mradi huo wa kilimo cha mpunga katika mabonde ya Mahekani, Tomokani, Mkanyageni, Mkuruwinda, Ndagoni, Mbuyuni Dole, Kichakani Bumbwisudi, Shamba ndogo, chemchem, kipanga na saraya.



Kwa upande wake mkulima wa bonde la mahekani, Bw. Abdalla Haji Abdalla amesifu juhudi za viongozi wa jimbo la Bububu kwa kuwajali wakulima wa jimbo hilo na kuelezea kuwa yeye ni mmoja kati ya watu walionufaika na mradi wa kilimo cha mbunga kwa awamu mbili zilizopita.




About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search