Gumzo: Hatua ya Jeshi la Polisi kutaka kumzuia Sheikh Ponda kutoa ujumbe wake...Je haki imetendeka? ...#share
Ni kama Filamu, Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia Sheikh Issa Ponda kuwatoroka askari polisi zaidi ya kumi waliotaka kumkamata.
Sheikh Issa Ponda akizungumza na waandishi wa habari
Tukio hilo lilitoka jana majira ya saa tano asubuhi jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Iris baada ya askari polisi kuvamia katika mkutano wa waandishi ambapo Sheikh Ponda alikuwa akitoa taarifa mbalimbali kutokana na matukio yanayoendelea ikiwamo mwenendo mzima wa mauaji, maiti kuokotwa, raia na viongozi kadhaa kutekwa na kupotea.
‘’Inaonekana baadhi ya askari polisi hawamfahamu sheikh Ponda kwani amewapita hapa wakiwa wanarandaranda na kutoka nje na kutokemea upande wa kulia wa hotel ya Iris.’’
Shuhuda alisema Sheikh Ponda alipishana na baadhi ya askari wanne ambao ndio wanaomjua vizuri kwa yeye kutumia njia ya miguu (ngazi) huku askari kanzu wakitumia lifti hotelini hapo.
Awali katika mkutano huo, Sheik Ponda alisema Watanzania wamekata tamaa na usalama wao na wanaishi kwa hofu na kwamba kama Serikali inawajibika ipasavyo matukio hayo yasingekuwepo.
‘’Serikali imekuwa ikiwaandama baadhi ya viongozi wa dini na wa vyama vya siasa hasa vya upinzani, wakati viongozi hao ndiyo wanaoikumbusha serikali wajibu wake na sasa wamekuwa wakifikwa na hatari ikiwamo kupata vilema vya kudumu.’’ Na kuongeza ‘’Mimi binafsi nilipigwa risasi hadharani mwaka 2013 na hivi sasa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Tundu Lissu .’’
Pia Sheikh Ponda aliiomba Serikali kuacha kuwazuia viongozi wa upinzani kuzungumza mambo mbalimbali yahusuyo nchi.
‘’Serikali imezuia haki za kidemokrasia kwa viongozi wa upinzani. Imezuia kufanya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani.’’
Awali Polisi walifika hotelini hapo wakiwa na gari mbili aina ya Defender wakiwa na silaha za moto kwa lengo la kumkamata Sheikh Ponda na kumzuia asizungumze na waandishi wa habari.
Wakati huo huo, waandishi watatu kutoka vyombo mbalimbali vya habari walikamatwa na polisi hao na kupakiwa garini na kupelekwa mahala kusikojulikana.
Kukamatwa kwao kulitokana na hatua yao ya kuwapiga picha polisi na gari zao na pia kuangali kilichozungumzwa na Sheikh Ponda.
Hata hivyo wakati tunarusha habari hii, waandishi hao waliachiwa huru baada ya kushikiriwa kwa saa tatu
Tundu Lissu ampa ujumbe mzito Shrikh Ponda
KABLA ya uvamizi huo Sheikh Issa Ponda alisema Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu ameahidi kuendelea na harakati za ukombozi na kupigwa kwake risasi kumemuongezea ujasiri zaidi.
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu
Ponda alisema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari na kusema kwamba afya ya Lissu inaendelea kuimarika.
‘’Hivi karibuni nilikuwa nchini Kenya alikolazwa Lissu kumjulia hali yake, kumuombea dua na kumjengea matumaini ya afya yake na matumaini endelevu ya harakati zake za umma na kujenga mazingira ya kutosha ili niweze kuzungumzia ipasavyo matukio ya mauaji, kuokotwa kwa maiti na kubanwa kwa uhuru wa viongozi na raia kuzungumza na kukemea maovu .’’
Alisema walizungumza vya kutosha na kwamba Lissu ameahidi pindi atakaporejea nchini ataendeleza mapambano na kamwe hawezi kukaa kimya.
‘’Amenieleza kazi muhimu anazofanya akiwa pale kitandani huku akiamini damu yake na yangu na zingine zitakazomwagika kwa namna hii zitawalipa watanzania kwa kupata uhuru wa kweli wenye thamani.’’ amesema
Sheikh Ponda alisema amehimizwa na Lissu mshikamano huku akiwa na matumaini ya kuwepo watu kama yeye wenye fikra na matumaini ya kuifikisha nchi sehemu salama.
Amesisitiza na kuwataka Watanzania kuwa na nguvu ya pamoja katika kutetea maslahi ya taifa.
‘’Wanaoamini hali iliyopo sasa inatokana na serikali kushindwa kutekeleza wajibu wake tuunganishe nguvu kuhakikisha serikali inatekeleza wajibu wake.’’
Sheikh Ponda aliwataka viongozi wa dini, wasomi, viongozi wa vyama vya upinzani na viongozi wa CCM waiambie Serikali ukweli.



No comments:
Post a Comment