Jamali Malinzi wenzake mambo bado ‘magumu’..Soma habari kamili na Matukio360..#share
Na Salha Muhamed
NDIVYO unavyoweza kusema kuwa Jamali Malinzi mambo yake bado ni magumu kufuatia mawakili wake wa utetezi kudai hawaruhusiwi kumuona pamoja na wenzake.
Raisi wa Zamani wa TFF Jamali Malinzi (katikati) akiwa na wenzake mahakamani. (Picha na Makataba)
Malinzi ambaye alikuwa rais wa chama cha mpira wa miguu Tanzania (TFF) na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha.
Leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mawakili hao wamesema hawaruhusiwi kuwaona wateja wao na kwamba upelelezi wa kesi hiyo kwa upande wa Takukuru umekamilika lakini jalada hilo bado limekwama kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Wakili wa utetezi Richard Rweyongeza ameyasema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai kueleza kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Rweyongeza amedai wiki iliyopita walipewa taarifa kuhusu uwepo wa jalada la kesi hiyo na wao hawana ugomvi na upelelezi, lakini wanapata tabu ya kuelewa kinachoendelea kwa DPP.
Amesema wameomba ahirisho fupi ili kuona nini kitatokea kwa kuwa makosa yao hayana dhamana.
Amedai hatua ya kuomba ahirisho fupi inatokana na wakati mgumu wanaoupata, ikiwamo kuzuiwa kuwaona wateja wao wakiwa mahabusu.
Wakili Swai amedai pande zote mbili zilifatilia kwa DPP ili kuhakikisha kesi hiyo inasikilizwa, hivyo wanaomba muda angalau wa wiki mbili.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 27/2017 huku akiutaka upande wa mashtaka ufike na jibu sahihi ili ipangwe tarehe kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga ambao wakikabiliwa na mashitaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani, 375,418.
Miongoni mwa mashitaka hayo ni inadaiwa, katika mashitaka ya kwanza kuwa Juni 5, mwaka jana, maeneo ya jiji la Dar es Salaam, Malinzi na Selestine walighushi nyaraka ya maazimio ya kamati tendaji ya Juni 5, mwaka jana kwa lengo la kuonesha kuwa kamati hiyo ya TFF imelenga kubadili mtia saini wa shirikisho hilo katika akaunti za benki kutoka Edgar Masoud kwenda kwa Mwanga.



No comments:
Post a Comment