Jambazi aliyempiga risasi Meja General Kariongo auwawa...Soma habari kamili na Matukio360..#share
Na Salha Mohamed
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuwaua majambazi wawili akiwamo mtuhumiwa aliyeshiriki tukio la kumvamia Meja Generali mstaafu wa Jeshi la Wananchi(JWTZ), VIcent Kariongo Septemba 11, 2017.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Lazaro Mambosasa.
Pia jeshi hilo limefanikiwa kupata silaha aina ya SMG na risasi 19, maganda 2
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema majambazi hao waliuawa Oct 11, 2017 majira ya saa nne usiku, maeneo ya Mbezi Mshikamano kwa Mgalula.
Amesema walipata taarifa kutoka kwa Francis Minde(30), mfanyabiashara ambaye anamiliki duka la vitu mchanganyiko, kwamba majambazi hao walifika katika duka lake wakitumia pikipiki aina ya Boxer nyeusi.
"Pikipiki hiyo haikusomeka namba ambapo walimuliza kama kuna huduma ya M-Pesa na Tigo-Pesa na kuwajibu kuwa hakuna huduma hiyo ambapo aliwatilia mashaka huenda si watu wazuri na kutoa taarifa Polisi,"amesema.
ACP Mambosasa amesema mara baada ya kupata taarifa hizo askari walikwenda eneo hilo na kuiona pikipiki ikiwa imeegeshwa gizani ikiwa na watu watatu, ambapo askari waliwaita watu hao ili kuwahoji lakini watu hao walianza kukimbia huku wakifyatua risasi.
Amesema risasi hizo zilifyatuliwa upande waliopo askari, hivyo askari nao walijibu mashambulizi na kufanikiwa kuwajeruhi majambazi wawili, mmoja kati yao alifanikiwa kukimbia na pikipiki waliyokuwa nayo.
"Eneo la tukio ilikutwa Silaha aina ya SMG yenye namba UC59821998 ikiwa na magazine mbili, magazine moja ikiwa na risasi kumi na tisa (19) na nyingine ikiwa tupu na maganda kumi na tatu (13) ya risasi aina ya SMG,"amesema.
Mambosasa amebainisha majeruhi wote wawili walifariki dunia wakiwa njiani kuelekea Hospitali ya Mwananyamala jijini humo, huku kukiwa askari aliyeumia au kujeruhiwa.
"Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala na jitihada za kumtafuta jambazi aliyekimbia zinaendelea,"amesema.
Katika hatua nyingine Jeshi hilo, walifanikiwa kuzima mpango wa majambazi kutaka kuiba katika Bar ya Tumaini wakiwa na gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 563 CAH rangi ya Blue.
Amesema tukio hilo limetokea Octoba 10 mwaka huu, maeneo ya Mbezi Luis, Tegeta “A” ambapo gari hilo lilikuwa limetolewa viti vyote vya nyuma na kubaki siti ya dereva na abiria, lengo likiwa ni kupakia vitu ambavyo wangeiba kwenye Bar hiyo.
"Wakati wakiendelea na uvunjaji askari walifika eneo la tukio na baada ya kugundua askari wamefika majambazi hao walifanikiwa kukimbia na kutelekeza gari hilo.
"Majambazi hao hawakufanikiwa kuchukua mali yeyote na gari lipo kituo cha Polisi. Ufuatiliaji unaendelea wa kujua mmiliki wa gari lililotumika katika tukio hilo,"amesema.
Wakati huo huo, Mambosasa amesema wamefanikiwa kuwafikisha mahakamani madereva 15 kutokana na kosa la kutovaa helment huku likikusanya sh mil 466 kutokana na tozo za makosa ya barabarani.
"Idadi ya yaliyokamatwa yalikuwa 14,340,Pikipiki 413,Daladala zilizokamatwa 5,024 Magari mengine (binafsi na malori) 1,205,Bodaboda waliofikishwa Mahakamani kwa makosa ya kutovaa helmet na kupakia mishikaki 15,"amesema.
Amesema jumla ya makosa yaliyokamatwa yalikuwa 15,545 ambapo magari yaliyokamatwa kutokana na Kuchelewa kulipa tozo kwa zaidi ya siku 7 yalikuwa 2,832 huku Kiasi kilicholipwa kikiwa sh mil 264.7.



No comments:
Post a Comment