JPM ampa mtihani Waziri Prof. Kabudi...Soma habari kamili na Matukio360.#share

RAIS John Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi kuunda timu zitakazoshughulikia biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi pamoja na migodi mingine ya dhahabu haraka iwezekanavyo ili nchi iweze kunufaika ipasavyo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp. Profesa John L. Thornton akiwa na Afisa Uendeshaji wa Barrick Gold  Richardc William huku Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Palamagamba Kabudi na Florens Luoga nao pia wakiweka saini ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na  timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam.

Agizo hillo Rais Magufuli amelitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya majadiliano kati ya Tanzania na timu ya wawakilishi wa kampuni ya Barrick Gold inayomiliki migodi ya madini hapa nchini ambayo yamekamilika na makubaliano kati ya pande hizo kutiwa saini mbele yake.

“Nataka machimbo yote ya dhahabu mchakato kama huu ufanyike, pia nakuagiza Prof. Kabudi biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi nako ni lazima kufuate utaratibu huu,
asiyetaka aondoke” amesema Rais Magufuli.

Aidha  amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi badala ya baadhi yao kuzibeza kwa kuwa zina manufaa kwa taifa na wananchi wake. 

Amezipongeza timu zote mbili yaani Tanzania na Barrick Gold Corporation kwa kazi kubwa ziliyofanya kufikia makubaliano hayo na kwa kipekee amempongeza Prof. Thornton kwa nia yake thabiti ya kukubali kufanyika kwa mazungumzo na kukubali mambo yaliyofikiwa.

Rais Magufuli amesema makubaliano hayo yataisaidia nchi kuzalishaji ajira zaidi, kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha za kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi na yanajenga msingi imara ambao utaiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake za madini.

Timu ya Barrick Gold Corporation ilikuwa imeongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo Prof. John Thornton wakati timu iliyowakilisha Serikali ya Tanzania imeongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi.

Miongozi mwa mambo waliyokubaliana ni kutekeleza mwelekeo mpya wa biashara ya madini ambapo kutakuwa na mgawanyo sawa wa faida (yaani Tanzania kupata asilimia 50 na Barrick Gold Corporation kupata asilimia 50 ya faida) na kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini iliyopo Tanzania ambayo itakuwa na makao makuu yake Mwanza na ofisi ndogo Dar es Salaam nchini Tanzania badala ya nchini Uingereza.

Mengine ni kufunga ofisi za uhasibu na fedha zilizopo Johannesburg Afrika Kusini na kuhamishia Tanzania na kutekeleza masharti yote ya mabadiliko ya sheria mpya ya madini na rasilimali za nchi ya mwaka 2017. 

Aidha, Barrick Gold Corporation imekubali kuwepo kwa wawakilishi wa Serikali katika bodi za migodi yake yote hapa nchini, kazi mbalimbali za kwenye migodi kufanywa na kampuni za Kitanzania, Migodi kutoa ajira za kudumu kwa wachimbaji, wachimbaji hao kuishi majumbani kwao badala ya kuishi kwenye makambi ya migodi na mashauri yote ya kesi mbalimbali kufanywa hapa nchini.

Kampuni ya Barrick Gold pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani Milioni 300 sawa na takribani Shilingi Bilioni 700 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo.

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo Prof. Thornton amempongeza Rais Magufuli kwa msimamo wake unaojenga misingi ya biashara ya kuaminiana na uwazi, ambayo ni muhimu na ya namna
yake kwa biashara katika karne hii ya 21. 

Prof.Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano haya na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimlaki  Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp.Profesa John L. Thornton alipokutana nae wakati wa kupokea ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na  timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search