Nyalandu ajiuzulu Ubunge, ang'atuka CCM kujiunga CHADEMA...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu amejiuzulu ubunge, nafasi zake zote CCM na ameomba kujiunga na CHADEMA

Lazaro Nyalandu
Leo jijini Arusha akitangaza uamuzi huo, Nyalandu amesema ‘nimeamua kujiuzulu nafasi  yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017.

‘Halikadhalika, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge,Job Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa.’

Amesema uamuzi wake huo ni kutoridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.

VILEVILE, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.

MIMI Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA,  kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali. AIDHA, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere.

Hivyo basi, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya KIKATIBA, natangaza KUKIHAMA Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii, na nitaomba IKIWAPENDEZA wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, basi waniruhusu kuingia MALANGONI mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru wa mawazo.


VILEVILE, nimemua kujiuzulu KITI Cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa UCHAGUZI mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua ITIKADI wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania. Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, SOTE kama TAIFA tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu. Ni maombi yangu kwa MUNGU kuwa Haki itamalaki Tanzania. Upendo, amani na mshikamano  wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za Kisiasa, na makabila yote nchini uimarike. Tushindane kisera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu, na TAIFA lililo imara na nchi yenye MAADILI.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search