Serikali kuanzisha operesheni maalum kudhibiti uchafu...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Hussein Ndubukile
SERIKALI imesema kuanzia Novemba Mosi hadi Disemba 31,2017 itaendesha oparesheni maalum ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira nchini kwa lengo lakukabiliana na madhara yatokanayo na mvua.


Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kange Lugola wakati alipotembea eneo la Tandale kwa Mtogole wilayani Kinondoni ambalo limeathirika na Mafuriko.

Amesema tatizo la mafuriko katika eneo hilo na maeneo mengine ya nchi yanachangiwa na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na takataka zinazotupwa kwenye mifereji, mabonde na mito na kwamba wakati mvua zinanyesha maji hushindwa kupita kutokana na njia za kupitisha maji hayo kuziba.

“ Wote tunatambua mafuriko yanasababishwa na nchi zilizoendelea kuchafua mazingira kina cha Bahari ya Hindi kinazidi kuongezeka ndio maana utaona tumejenga kuta maeneo ya mwambao wa bahari kukabiiliana na hali hii,” amesema.

Amebainisha kuwa mafuriko yanapotokea huathiri miundo mbinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, madaraja na majengo kuzolewa na maji na kuongeza oparesheni hiyo itaendana na uzibuaji wa takataka zilizoziba kwenye mitaro, mifereji na kingo za mito.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Kangi Lugola akisafisha eneo la Mto Ng’ombe kuashiria uzinduzi wa operesheni maalum ya miezi miwili ya kusafisha mito nchi nzima
Amesisitiza kuwa wananchi wamekuwa wakitimiza wa wajibu wa kukusanya taka kwa ajili ya kubebwa na magari ya taka ya manispaa ila watendaji wa manispaa wanashindwa kuwajibika kusababisha wananchi kuchukua uamuzi wa kuzitupa taka hizo kwenye maeneo yasiyotakiwa.

Amewaagiza viongozi wote wa halmashauri za majiji, manispaa na wilaya kushiriki kikamilifu oparesheni hiyo kwa kuhakikisha maeneo yote hatarishi yanazibuliwa kwa kugawa vitendea kazi vya kutosha kupunguza mafuriko.

Amefafanua kuwa baada ya miezi miwili ukaguzi utafanyika katika maeneo yote kuona kwa kiasi gani oparesheni  imefanyika na kwamba Wakurugenzi watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watawajibishwa.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Tano inawajali na kuwatahamini wananchi wake hivyo haitakubali kuona afya za wananchi zinaathiririka kutokana na magonjwa ya milipuko yakiwemo ya homa ya matumbo, kuhara na Kipindupindu.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Dkt. Aaron Kagumrujuli amesema Serikali za mitaa zinashindwa kuwasimamia wakandarasi waliopewa jukumu la kubeba taka kwenye mitaa husika kiasi cha kuchangia uchafuzi huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Muhalitani, Sudi Makamba amesema wananchi wanakusanya takataka za kuziwekwa sehemu husika ila taka hizo zimekuwa zikikaa muda mrefu bila kuzolewa na magari ya taka.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Ali Maua, Juma Ulole Ulole amesema takataka zinazoleta madhara eneo hilo zinatoka mbali na kuiomba Serikali kuwaletea magari ya taka kupunguza mrundikano.


Amesema suluhisho la mafuriko katika eneo hilo ni kuuchimba na kupanua mto unaopita eneo hilo.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search