Serikali yatangaza ajira 400 TRA...Soma habari kamili na Matukio360..#share
KATIKA kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumiahi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) serikali inatarajia kuajiri wafanyakazi 400 katika kipindi kifupi kijacho.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (aliyesimama) akizungumza na
viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga kuhusu nia
ya Serikali katika kuhakikisha kodi ya majengo na mabango inakusanywa
kikamilifu kwa manufaa ya wananchi na Taifa, alipofanya ziara ya kikazi
katika mkoa huo.
Hayo
yamebainishwa jana mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa TRA katika ziara yake ya kikazi ya
kukagua utendaji wa Mamlaka hayo mkoani humo, amesema hatua hiyo
inatarajia kungeza ufanisi wa kazi na makusanyo ya kodi.
Dk. Kijaji
amesema kuwa taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi za ajira
zitatangazwa na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA kuwafikia watu
wengi zaidi na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.
“Tunatambua changamoto
ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ndio maana
tumeamua kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko kada nyingine
ili tuweze kuimarisha utendajikazi wa Mamlaka na hivyo kuongeza makusanyo
ya kodi zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo nchini” alisema Dk. Kijaji.
Alisema kuwa
pamoja na uhaba wa watumishi, anaamini kuwa lengo la mwaka huu la kukusanya
shilingi trilioni 17 ambazo Mamlaka hayo imepangiwa yatafikiwa na ikiwezekana kuzidi kwa kutumia wafanyakazi waliopo.
Dk.
Kijaji alitoa rai kwa wafanyakazi wa TRA kuwa waadilifu na kwamba atakayebainika
kukiuka maadili yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za kinidhamu na
kisheria.
Awali Meneja
wa TRA mkoa wa Shinyanga Jumbe Samson,
alieleza
kuwa mkoa wake umepangiwa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 18 na kwamba
wanauhakika wa kufikia lengo hilo kutokana na mikakati mbalimbali
waliyojipangia ikiwemo kusimamia ukusanyaji kodi kikamilifu katika sekta
ya madini.
Kwa
upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA Beatus Nchota alisema kuwa Mamlaka
yake imejiwekea mipango ya kufungua ofisi zake kila wilaya hapa nchini ili
kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa
mapato ya Serikali ili lengo walilopewa la kukusanya shilingi trilioni 17
liweze kufikiwa.
Mkuu wa
Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa
mkoa wa Shinyanga, alisema kuwa Serikali mkoani humo itahakikisha kuwa TRA
inatimiza malengo yake ya kukusanya kodi na kumhakikishia
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji kwamba watasimamia
kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Naibu Waziri
huyo aliwasisitiza watumishi wa TRA mkoa wa Shinyanga kuhakikisha
wanafanyakazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya
kukusanya Shilingi trilioni 17.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wengine wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga, alipofanya ziara ya kikazi kukagua namna Mamlaka hayo inavyokusanya kodi.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
No comments:
Post a Comment