Simba ikivaa Yanga Aveva, Kaburu mambo bado magumu..soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Mwandishi wetu
 WAKATI zikiwa simesalia siku chache watani wa jadi katika soka Simba na Yanga kuvaana rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake,Godfrey Nyange ‘Kaburu’ hadi sasa, jarada la uchunguzi la kesi inayowakabili ya utakatishaji wa fedha dola za kimarekani 300,000 bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ,(DPP).

Aveva na Kaburu wakiingia katika moja ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Wakili wa Serikali mkuu, Vitalis Peter ameeleza hayo leo kwa Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa na kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwalakini jalada la uchunguzi bado lipo kwa DPP na ameomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine.

Hata hivyo Wakili wa washtakiwa hao, Evodius Mtawala amedai kuwa upande wa mashtaka  Septemba 18,2017 ulitoa taarifa kuwa jalada la uchunguzi wa kesi hiyo lipo kwa DPP.

Mtawala amedai  tangu siku hiyo ni siku  37 zimepita hivyo ameiomba Mahakama iwahimize upande wa mashtaka kulifuatilia jalada hilo kwa DPP kwa sababu wateja wake wapo ndani na maisha yao yamekuwa ni kama yamesimama.

Akijibu hoja hizo za Wakili Mtawala, Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),Leonard Swai amedai kuwa ni kweli na kwamba wanajitahidi kulifuatilia lakini hadi sasa bado halijatoka kwa DPP.

Hata hivyo, Swai amedai   sheria haijampa muda DPP wa kukaa na jalada ila kwa upande wao ni kuhimiza tu.

Hakimu Nongwa baada ya kusikiliza hoja hizo, aliwataka upande wa Mashtaka walifuatilie na ameiahirisha kesi hadi Novemba 6,2017.

Evans Elieza  Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha USD 300,000.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.

Katika la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29,2016 Dar es Salaam  kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa  Machi 15,2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva  kujipatia USD 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

Simba ya Yanga zinatarajiwa kupambana Oktoba 28, 2017 katika uwanja wa Uhuru ‘shamba la bibi’ jijini Dar es Salaam



About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search