Uwanja wa ndege Sumbawanga kujengwa Disemba...soma habari kamili na Matukio360..#share
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa uwanja
wa ndege wa Sumbawanga utaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia mwishoni
mwa mwaka huu baada ya taratibu za kumpata mkandarasi kukamilika.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kushoto), akitoa
maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mkoa
wa Rukwa, Mussa Mchola (wa pili kulia),
wakati alipokagua Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga, Mkoani Rukwa.
Akizungumza
na wananchi wanaozunguka Uwanja huo Prof. Mbarawa amewahakikishia wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia
kutokana na kupisha ujenzi huo watalipwa fidia zao katika kipindi kisichozidi
miezi miwili kuanzia sasa.
“Jumla
ya wananchi 97, ndio wanaostahili kulipwa fidia na kiasi cha shilingi bilioni
3.3 kimetengwa na wataanza kulipwa hivi
karibuni kabla ya zoezi la ujenzi wa uwanja huo kuanza” amesema Prof. Mbarawa.
Amewataka
wananchi hao kuacha kupita katika uwanja huo kwani ni hatari kwa usalama wa ndege na usalama wa wananchi
wenyewe.
Ujenzi
wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga unajengwa kwa kiwango cha lami na kuongezwa
urefu kutoka kilomita 1.5 had 1.7 ili kuwezesha ndege kubwa zaidi kutumia
uwanja huo na hivyo kuufungua mkoa wa Rukwa na mikoa mingine hali
itakayochochea maendeleo na ukuaji wa uchumi kwa mkoa huo.
Kaimu
Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mkoa wa Rukwa, Mussa Mchola amemshukuru Waziri Prof.
Mbarawa kwa hatua ya kulipa fidia na kumhakikishia kuwa watamsimamia mkandarasi
huyo kikamilifu ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Katika
hatua nyingine Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof Mbarawa amekagua
Ujenzi wa Barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port KM 112 na mizani ya Singiwe
na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ambapo amemtaka mkandarasi China Railway 15, Bereau Group Corporation (CR15G) na Henan Provincial Newcentry Road na Bridge
Consultants Limited JV anaejenga kuongeza kasi katika maeneo korofi kabla ya
Mvua za masika kuanza.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mwl. Julieth Binyura amezungumzia umuhimu wa
ukamilishaji wa barabara hiyo utakavyonufaisha wilaya hiyo kwa kuwa
inaunganisha Wilaya hiyo na bandari ya Kasanga na mpaka wa Kasesha unaounganisha
Tanzania na Zambia na hivyo kuchochea uzalishaji na uchukuzi kati ya Tanzania,
Kongo na Zambia.
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iko katika mchakato wa kuunganisha kwa
kiwango cha lami barabara zinazoingia katika bandari za mipakani ili kukuza
huduma za uchukuzi kati ya Tanzania na nchi jirani kwa njia za magari, ndege na
meli.



No comments:
Post a Comment