Mahakama yapokea hati ukamataji mali za Wema ..soma habari kamili na Matukio360...#share

Na mwandishi wetu
MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu imepokea hati ya ukamataji mali iliyojazwa katika upekuzi nyumbani kwa msanii wa filamu,Wema Sepetu kama kielelezo. Mbali na Wema, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Angelina Msigwa  na Matrida Seleman Abbas.


Wema Sepetu kushoto akitinga Mahakamani

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba ametoa uamuzi huo leo kwa kuwa upekuzi huo ulifanywa nyumbani kwa Wema na si mwilini mwa Wema.

Amesema upekuzi huo ungefanywa maungoni mwa Wema ni lazima apekuliwe na mwanamke.

Uamuzi huo imefuatia   baada ya upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula kuiomba Mahakama ipokee hati hiyo ya ukamataji Mali kama kielelezo huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala ukipinga.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 16,2017 na kwamba siku hiyo upande wa mashtaka upeleke mashahidi wao wote.

Katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa Wema inadaiwa ilikutwa  misokoto inayodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya bangi.

Katika ushahidi uliotolewa na Inspekta Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Wille (43) kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi  wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya  Dar es Salaam alidai katika upekuzi huo walifanikiwa kukuta misokoto inayodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya bangi.

Wille alidai Februari 4,2017 anaikumbuka kwa sababu aliitwa na Mkuu wake wa kazi  na kupewa kazi ya kufanya upekuzi  nyumbani kwa Wema na aliongozana na WP Mary, Koplo Robert, PC Hassan na dereva kuelekea Unonio anapoishi Wema ili wakaufanye upekuzi huo.

Inspekta Wille alidai  kuwa walipofika  nyumbani kwa Wema huko Ununio waligonga mlango na  kwamba waliwakuta wasichana wawili ambao ni wafanyakazi  wa Wema  na wakaomba  waitiwe mjumbe wa nyumba kumi Steven Noho wakaitiwa.

Shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka alidai kuwa walimueleza kuwa wamekwenda nyumbani kwa Wema kwa nia ya kufanya upekuzi nyumbani kwa Wema na wanatafuta dawa za kulevya na kitu chochote ambacho wangekitilia shaka.

Wema alisema dada yake awepo ili ashuhudie upekuzi huo, dada yake alifika na tukapekuwa  ambapo upekuzi wetu ulianzia jikoni  ambapo juu ya kabati la vyombo  tulifanikiwa kukuta msokoto mmoja unaodhaniwa kuwa ni bangi na karatasi ya kusokotea, Alieleza shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka.

Katika chumba cha Wema ambacho anahifadhia nguo na vitu vyake vingine mlango ulikuwa umefungwa lakini wafanyakazi wake walituletea, tukafungua  na tukafanikiwa kukuta vipisi na msokoto unaodhaniwa  kuwa ni bangi dirishani.”Alieleza shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka.

Akiendelea kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo, Inspekta Wille alidai kuwa upekuzi huo uliendelea  katika chumba cha wasichana wa kazi wa Wema, walifanikiwa kukuta kiberiti ambacho ndani yake kulikuwa na msokoto ambao unaonekana  umeishavutwa.

Alidai kuwa baada ya kufanya upekuzi huo, walisaini hati ya ukamataji wa mali ambapo yeye aliisaini,  Wema mwenye aliisaini, wafanyakazi wake, dada yake, pamoja na mjumbe wa eneo la Unonio.

Aliongeza kuwa baada ya hapo walienda kituoni na kumkabidhi mtunza vielelezo, Robert.

Inadaiwa  kuwa  Februari 4,2017 katika Makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio  washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.


Kwa upande wa Wema yeye anadaiwa kuwa Februani Mosi, 2017 katika  eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam,  alitumia dawa za kulevya  aina ya Bangi.

Wema ni miongoni mwa watu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda wakituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Inadaiwa kuwa Februari 3, 2017, Wema alijipeleka mwenyewe katika Kituo cha Polisi Kati ambapo alikamatwa.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search