Mali za meneja wa Diamond kupigwa mnada...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na mwandishi wetu
KAMPUNI ya Tiptop Connection Company Limited inayomilikiwa na Hamis Shaban Taletale ‘Babu Tal’ ambaye ni Meneja wa Diamond Plutnam na Idd Shaban Taletale, iko hatarini kupigwa mnada kwa kushindwa kulipa fidia ya milioni 250.



 Msanii na mkurugenzi wa kampuni ya, TipTop Conection Ltd, Hamisi Shabani 'Babu Tale'
Tayari kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart & Co Ltd imewapa siku 14, Babu Tale na nduguye kama wakurugenzi wa kampuni hiyo  kutaja mali za kampuni hiyo, au wao wenyewe wawe wamelipa pesa hizo ndani ya muda huo.

 Hatua hiyo ya Yono ni utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyoamuru kampuni hiyo kumlipa fidia ya milioni 250 Mhadhiri wa Dini ya Kiislama, Sheikh Hashim Mbonde.

Mahakama Kuu, Februari 18, 2016 iliamuru kampuni hiyo kumlipa fidia hiyo Sheikh Mbonde kwa kutumia kazi zake za masomo na mahubiri kibiashara bila ridhaa wala makubaliano naye, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria,


Baada ya hukumu hiyo, Sheikh Mbonde alifungua maombi ya utekelezaji ndipo Juni 9,2017 Naibu Msajili wa Mashauri aliwaamuru Babu Tale na ndugu yake waweke wazi mali za kampuni hiyo, au walipe fidia hiyo.

Pia katika uamuzi huo Naibu Msajili Mashauri aliamuru kuwa kama watashindwa kutaja mali hizo wala kulipa wenyewe fidia hiyo basi mali zao zitapigwa mnada na kama hawana mali basi watafungwa jela kama wafungwa wa kesi ya madai.

Leo Sheikh Mbonde amesema  tayari wameshawapelekea kina Babu Tale taarifa hiyo, na kwamba taarifa hiyo ilikabidhiwa na Meneja Masoko wa Yono, Kene Mwankenja, kwa Kaimu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpakani iliyopo Kata ya Kwembe, wilaya ya Ilala, John Wilson, ili awafikishie.

 Katika kesi ya msingi namba 185 ya mwaka 2013, Sheikh Mbonde alikuwa akidai fidia ya jumla ya milioni 750 kwa kutumia kazi zake za mihadhara kibiashara bila idhini yake kinyume cha makubalino.

Sheikh Mbonde alikuwa anaiomba mahakama imwamuru mdaiwa (Tip Top Connection) imlipe fidia ya jumla ya Smilioni 700 ikiwa ni fidia ya hasara  na kuwa faida aliyotarajia kuipata kutokana na mauzo ya kazi zake hizo na milioni 50.

Kwa mujibu wa hati ya madai na kwa mujibu ushahidi wa upande madai wakati wa usikilizwaji, Juni 6, 2013 Sheikh Mbonde aliingia makubaliano na kampuni hiyo, kutumia kazi zake za mawaidha, kwa kuzalisha, kurekodi na kuzisambaza.

Walikubaliana kwamba kampuni italipia gharama za kurekodi masomo na mafundisho ya mihadhara yake, kumnunulia gari, kumjengea nyumba na kuzitangaza kazi zake kupitia vyombo vya habari.

Pia walikubaliana kuwa baadaye wangeingia makubaliano ya kugawana faida ambayo ingepatikana kutokana na mauzo ya kazi hizo na siku hiyohiyo ilimlipa milioni 2  na ikamnunulia kanzu na kofia kwa maandalizi ya kurekodi mkanda wa video wa kazi hizo katika mfumo wa DVD.

Baadaye katika tarehe tofauti  na katika misikiti tofauti kampuni hiyo ilirekodi masomo mbalimbali aliyokuwa akiyatoa na baada ya kukamilisha kurekodi masomo saba, kampuni hiyo ilimkatia mawasilino.

Baadaye mmoja wa maafisa wa mdaiwa, Adam Waziri alimweleza mdai kuwa wamesitisha mpango wa kuendelea na kazi hiyo na kwamba mdai hakuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na maelezo hayo.

Hata hivyo  Agosti 9, 2013, wakati mdai akiendesha mhadhara Bahi Dodoma, alibaini kuwa DVD za masomo yake zilikuwa zikiuzwa sokoni Dodoma na katika  mikoa mbalimbali kama vile Mbeya, Tanga na Dar es Salaam, bila ridhaa yake wala makubalino.

DVD hizo kwa mujibu wa hati hiyo zilikuwa ni za masomo mbalimbali aliyokuwa ameyatoa na kwamba makava ya DVD hizo zilikuwa na nembo na namba za simu, za maafisa wa mdaiwa.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search