Malkia pembe za ndovu alalamika mahakamani...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Abdulrahim Sadiki
RAIA wa China Yang Feng Glan ‘Malkia wa Pembe za Ndovu’, ameilalamika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya mashahidi wa upande wa mashtaka kutofika mahakamani.


Yang amelalamika leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi akidai Jaji Mkuu ameagiza kesi za muda mrefu lazima zimalizwe mwaka huu.

 " Rais Magufuli anasema hapa kazi tu, Nikasema sasa mahakama ile kazi haipo kwa haraka, nipo mahabusu naumwa moyo najitahidi nakuja," ameeleza Yang.

Ameomba mashahidi katika kesi hiyo wafike na si kila siku kutoa udhuru wa kuumwa.

Yang aliyaeleza hayo baada ya Wakili Wankyo Simon kudai kuwa shahidi waliyemtarajia kutoka ushahidi katika kesi hiyo bado anaumwa na akaomba ipangiwe tarehe nyingine na kwamba siku hiyo wanaamini atakuwa vizuri.

Wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko, aliomba mahakama iliangalie hilo na kuwa waendelee na mashahidi wengine wa upande wa Mashtaka ili kuokoa muda.

Wakili Wankyo alidai kuwa katika hali ya kawaida ni lazima shahidi huyo amalizie kutoa ushahidi wake.

Hakimu Shaidi aliutaka upande wa Mashtaka kupelekwa mashahidi  kama huyo hatakuwa hajatengemaa.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Novemba 21,24,27,28,29,30 na Desemba Mosi, 2017.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Salvius Matembo na Philemon Manase ambao kwa pamoja, wanadaiwa kuwa  kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22,2014  walijihusisha na biashara  ya nyara za serikali.

Katika kipindi hicho washtakiwa hao wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilogramu 1889 zenye thamani ya Sh 13 bilioni  bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22,2014  kwa makusudi raia wa China, China, Yang Feng Glan  aliongoza na kufadhiri vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande hivyo 706 vya Meno ya Tembo bila ya kuwa na kibali chochote kile kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Kwa upande wa washtakiwa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za serikali kwa kukusanya, Kusafirisha na Kuuza Meno ya Tembo kwa nia ya kujipatia faida.

Ilidai kuwa Mei 21, 2014 katika eneo la Sinza Palestina wilaya ya Kinondoni mshtakiwa Manase alitoroka chini ya ulinzi halali wa askari wa Jeshi la Polisi D 7847 Koplo Beatus ambaye alikuwa akimshikilia kwa makosa ya kujihusisha na biashara za nyara za serikali.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search