Matibabu Harbinder Sethi utata! soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Abdulrahim Sadiki
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili(MNH) imedaiwa kushindwa kumfanyia Harbinder  Sethi operesheni ya puto lililopo tumboni mwake.Hata hivyo Takukuru imepinga jambo hilo ikidai Muhimbili inauwezo wa kumtibu.

Harbinder  Sethi wa kwanza kulia

Hayo yamesemwa leo na wakili wa Sethi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuiomba mahakama hiyo mteja wao atibiwe na daktari maalum kutoka nchini Afrika Kusini.

Wakili Joseph Sungwa amewasilisha ombi hilo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Huduma Shaidi mara baada ya mwendesha mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai kudai  kesi ilipangwa kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Wakili Sungwa aliwasilisha ombi hilo alieleza kuwa anaomba Sethi kutibiwa na Daktari huyo maalum wa Afrika Kusini juu ya puto ambalo linaisha muda wake  kwa madai ya kwamba Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  hawawezi kufanya upasuaji huo.

Wakili Sungwa amedai   mteja wake baada ya kufanyiwa vipimo Muhimbili, walimweleza hawawezi kufanya upasuaji wa puto.

Hivyo, Wakili huyo aliomba daktari huyo wa Afrika Kusini aweze kuja  kumtibia Sethi ama asafirishwe Afrika Kusini kwa matibabu.

Swai alipinga ombi hilo, akidai Muhimbili  haijashindwa kumfanyia upasuaji wa puto Seth, bali yeye mwenyewe ndiyo anajichelewesha kutokana na kutaka uwepo wa daktari wake wa Afrika Kusini.

Alidai kuwa  mahakama hiyo ilikwishatoa amri Sethi  apelekwe Muhimbili kwa matibabu, amri ambayo ilitekelezwa na hoja ya kwamba puto lililoko tumboni kwake limeisha muda halijathibitishwa.

Alidai ripoti ya daktari ni siri kati ya daktari na mgonjwa, hivyo hawezi kuisemea kwa kuwa hawajaisoma lakini wanapata shaka la maelezo ya wakili wa Sethi  kuwa  Muhimbili imeeleza kuwa  haina utaalamu wa kumfanyia upasuaji wa puto.

Swahi amesema taarifa za Jeshi la Magereza ambako Sethi  yupo na ripoti ya Hospitali ya Muhimbili imepitia gereza alilopo na kwamba ni kweli hospitali hiyo ipo tayari na ina uwezo wa kumfanyia upasuaji huo.

Mshtakiwa alitueleza Magereza kuwa anahitaji daktari wake wa Afrika Kusini aje kumtibu, lakini siyo kweli kwamba Tanzania hatuna uwezo wa kumtibu.

Alidai kuwa suala hilo  linahitaji utaratibu kwa sababu linahusisha taasisi tofauti ambazo ni Magereza, Muhimbili na serikali.

Kuhusu hoja ya Sethi  kupelekwa Afrika Kusini, Swai alidai  ni ngumu na haiwezekani  kabisa na hawaoni sababu ya kupelekwa huko wakati Muhimbili wamethibitisha wanauwezo wa kumfanyia upasuaji wa puto.

Akielezea upelelezi wa kesi hiyo, Swai alidai wapo katika hatua nzuri ambapo wanataka kwenda mahabusu kuchukua maelezo ya onyo ya washtakiwa hao.

Swai alidai amri ikitoka wachunguzi wataenda kuchukua maelezo yao.

Hoja ya upelelezi iliibuliwa na Wakili Michael Ngalo, alidai upelelezi umechukua muda mrefu ni takriban miezi mitano sasa haujakamilika na washitakiwa wapo mahabusu.

Baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote husika, Hakimu Shaidi alisema juu ya mshtakiwa ana uwezo wa kutibiwa Muhimbili ama la, mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri yoyote hivyo wawasilishe maombi Mahakama Kuu.

Pia, Hakimu Shaidi alikubaliana na ombi la wachunguzi kwenda kuchukua maelezo ya onyo ya washitakiwa mahabusu. Hivyo siku ya Jumatatu watachukuliwa maelezo hayo SAA 4 asubuhi.

 Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 24, mwaka huu.

 Katika kesi hiyo, Sethi na James   Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.




About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search