NEC yaridhia uamishwaji vituo 21 vya kupigia kura Mbweni...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Hussein Makame-NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeridhia  uamuzi wa kuhamisha vituo 21 vya upigaji kura katika kata ya Mbweni, jimbo la Kawe, Kinondoni. na kwamba hatua hiyo imezingatia sheria na kanuni za uchaguzi.


Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Kailima Ramadhani akiwa na kitabu cha wageni kwenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Malindi Estate ambayo ipo kwenye nyumba ya mmoja wa wagombea wa Uchaguzi Mdogo wa Madiwani Kata ya Mbweni.Picha na NEC.

NEC imetoa msimamo huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi na vyama vya siasa wakilalamika kuamishwa kwa vituo nane  vya kupigia kura na kupelekwa katika kituo cha Polisi.
Pia kuhamishwa kwa vituo vingine 15 kutoka maeneo ya awali  jambo ambalo baadhi ya vyama havikukubaliana na uamuzi huo.

Jana Mkurugenzi wa Uchaguzi, NEC Kailima Ramadhani akiambatana na watendaji wengine wa Tume, walitembelea maeneo hayo na kujiridhisha mabadiliiko ya vituo yaliyofanywa na msimamizi wa uchaguzi yamekidhi matakwa ya kisheria.

 “Nimefika hapa jimbo la Kawe kata ya Mbweni, baada ya mwananchi mmoja kunitumia ujumbe akiniambia kuwa kuna chama kimoja kinachoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Madiwani wa Kata ya Mbweni kinalalamika kwamba Tume imehamisha vituo vya kupigia kura kiholela,” amesema Ramadhani.

Amesema chama hicho kimelalamika kuwa vituo hivyo vimepelekwa kwenye eneo la kituo cha Polisi, kwa hiyo huenda wapigakura wakanyimwa haki yao ya kupiga kura.

Kailima amesema alipowauliza watendaji wa Manispaa ya Kinondoni, majibu yao hayakumridhisha ndipo alipoamua kufika eneo la tukio.

“Kwanza wanalalamika kwamba vituo vilivyohamishwa ni 27, lakini ukweli ni vituo 21, vituo hivyo vimehamishwa kwa mujibu wa Sheria kwa sababu  Novemba mosi 2017, Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata aliviita vyama vinne na kufanya mkutano na aliwaambia tunavihamisha vituo hivyo kwa sababu mbalimbali.

“Sababu alizozitoa msimamizi wa uchaguzi ni kwamba vituo vinane  vilikuwa shule ya Sekondari New Era na vituo saba 7 vilikuwa jirani na nyumbani kwa mgombea ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na vituo sita vilikuwa kwenye eneo la Kanisa,” alifafanua Kailima.

Amebainisha kuwa kifungu cha 20 (2) cha Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2015 na Kifungu cha 21 cha Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa 2015, vinabainisha kuwa vituo vya kupigia kura havipaswi kuwa kwenye maeneo ya watu binafsi, kwenye maeneo ya ibada na kwenye kambi za jeshi.

Kutokana na msingi wa kanuni hizo, Kailima alithibitisha kuwa uamuzi wa kuvihamisha vituo hivyo kwenye maeneo hayo ambao umefanywa na  msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Kawe ni sahihi.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuri amesema malalamiko kuhusu kuhamishwa kwa vituo hivyo yalitolewa na chama kimoja kati ya vyama vinne vinavyoshiriki uchaguzi.

Uchaguzi mdogo wa kata hiyo unafanyika baada ya mahakama kutengua uchaguzi wa awali kutokana na ukiukwaji wa baadhi ya taratibu za uchaguzi.

Alifafanua kuwa hali halisi inaonesha kwamba kanuni  na taratibu za kupigia kura, haziruhusu kuweka kituo kwenye jengo la mtu binafsi,  na shule hiyo ambayo ilikuwa na vituo kadhaa ni shule ya mtu binafsi.


“Kwa hiyo kwa Uchaguzi huo wa mwaka 2015 kanuni hizo zilikiukwa sasa kwa uchaguzi huu kwa sababu tunataka tufanye uchaguzi kwa kufuata kanuni na sheria hatukutaka kuingia kwenye uvunjaji wa kanuni na taratibu,” amesema

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search