Operesheni kamata 'bodaboda' yaanza...soma habari kamili na Matukio360..#share
Na Salha Mohamed
JESHI la Polisi kikosi cha Usalama barabarani, limeanza
operesheni ya kukamata madereva pikipiki wanaovunja sheria .
MKUU wa kikosi cha Usalama wa Polisi barabarani, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Marisone Mwakyoma (katikati) akizungumza na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama katika Kanda hiyo yanayotarajia kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda Novemba 18/2017 katika viwanja vya biafra.
Agizo hilo limetangazwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani Kanda
ya Dar es Salaam, SSP Marisone Mwakyoma alipokuwa akizungumzia maandalizi ya
maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama yanayotarajia kuanza Novemba
18-23/2017.
"Tumeshaunda kikosi kazi kwa Kanda ya Dar es
Salaam, tumeanza operesheni, kwa dereva atakayekiuka sheria makusudi
tutamchukulia hatua kwake na kwa jamii
nzima, "amesema.
Amesema operesheni wanazofanya hadi sasa zimepunguza
ajali kwa asilimia 25.
Mwakyoma amefafanua kuwa wana kamera za kisasa zinazopiga
picha madereva watakaovunja sheria na kuwakimbia polisi hata nje ya eneo la
tukio.
"Hatuhitaji kuwakimbiza, tutawakamata huko huko,
"amesema kuongeza kuwa madereva
wanapaswa kusomea ili kujua mabadiliko ya sheria za barabarani.
Amesema dereva anapokamatwa na trafiki kwanza anapaswa
kujua kosa lake na kukubaliana nalo au kujitetea kabla ya kuandikiwa kulipa
faini.
" Hatuhitaji trafiki anayemwandikia mtu kosa moja
kwa moja, anapaswa kumwambia kosa gani amefanya, aridhike amwandikie au waende
mahakamani, "amesema.
Amesema jijini Dar es Salaam makosa yanayoongoza kufanywa ni kupakia mizigo
kwenye gari la abiria, kukatisha njia na kupita pembezoni mwa barabara.
Mengine ni ulevi, kutovaa sare, kutokuwa na tiketi na
kuendesha kwa mwendo hatarishi.
Maadhimisho
hayo yanatarajia kufunguliwa na Mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda katika viwanja
vya Biafra yenye Kauli mbiu 'Zuia ajali, Tii Sheria - Okoa maisha'
No comments:
Post a Comment