Vigogo NIDA waendelea kusota rumande...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Abdulrahim Sadiki
UPELELEZI wa kesi  ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya  bilioni 1.16  inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), Dickson Maimu na wenzake, bado haujakamilika.

Wa kwanza mbele ni Dickson Maimu ambaye aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya vitambulisho (NIDA)
 Leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakili mkuu wa serikali, Vitalis Peter amesema hayo kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Peter amedai  upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwa upande wa Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai amedai  jalada la kesi hiyo  limesharudi kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Hakimu Mwijage ameutaka upande wa Mashtaka ukamilishe upelelezi wa kesi hiyo ili washtakiwa kama walikula fedha za umma wafungwe au  hawajala waachiwe na si kila siku upelelezi haujakamilika.

Hakimu Mwijage ameiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6,2017 na kuutaka upande wa Mashtaka siku hiyo uje na kitu na siyo upelelezi bado haujakamilika.

Mbali ya Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa (NIDA), Avelin Momburi na Mkurugenzi wa TEHEMA, Joseph Makani.

Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers,  Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji,  George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 1,169,352,931.

Inadaiwa kwenye shtaka la kwanza Maimu na Mwakatumbula kati ya Januari 15 hadi 19,  mwaka 2010 katika makao makuu ya NIDA  wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo  walitumia madaraka  vibaya.

Wanadaiwa kuwa waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na  Benki Kuu ya Tanzania,    kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya NIDA na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 3,969,000.

Maimu na Mwakatumbula katika shtaka jingine wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8, bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Washtakiwa hao wawili wanadaiwa Juni 20, 2014 katika makao makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo mengine ya Sh6 milioni  kwa GIL bila ya kupiga  hesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 14, 661,676.76.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika makao makuu hayo ya NIDA kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni waliisababishia NIDA kupata hasara ya Sh 167,445,676.76.





About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search