Vigogo walia njaa mahakamani...soma habari kamili na Matukio360...#share

Na Abdulrahim Sadiki
MKURUGENZI wa Tathmini, Archard Alphonce Kalugendo (49) na Mthamini wa Madini ya Almas wa Serikali, Edward Joseph Rweyemamu (50) wamezidi kuiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu isaidie  familia zao kupata mishahara yao.

Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu
Washtakiwa hao, kupitia wakili, Nehemia Nkoko walitoa ombi hilo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Nkoko ameomba mahakama isaidie familia za washtakiwa hao kupata mishahara hiyo kwa sababu wana watoto ambao wanahitaji huduma na wanaugua.

"Tungependa washtakiwa wapate dhamana lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amewawekea zuio la dhamana hivyo tunaomba wapatiwe mishahara yao hata kwa kupitia dirishani halafu wao waendelee kushikilia hizo akaunti," ameeleza Nehemia.

Nehemia ameyaeleza hayo leo mara baada ya Wakili wa Serikali, Wankyo Simon kudai jalada la polisi la kesi hiyo lipo kwa DPP na kwamba tarehe ijayo wataeleza kwa ufasaha  upelelezi wa kesi hiyo umefikia wapi.

Kwa upande wa Wakili mwingine wa utetezi, Ludovick yeye alidai kuwa washtakiwa hao walishikiliwa polisi kwa takribani wiki tatu wakisema wanachunguza wakikamilisha watawapeleka mahakamani, tumaini la upande wa utetezi ni walipoletwa mahakamani upelelezi umekamilika.

Hivyo aliomba upande wa Mashtaka kueleza ni sehemu gani ambayo upelelezi bado kwa sababu wao wanaamini hadi washtakiwa hao wanaletwa mahakamani upelelezi umekamilika.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Wakili wa Serikali, Wankyo alimshauri wakili Nkoko kuandika barua kwa DPP ili aweze kushughulikia suala hilo.

Nehemia alisisitiza kuomba familia za washtakiwa hao zipatiwe mishahara hiyo kwa sababu chanzo chake kinajulikana kinatoka wapi na kwamba familia hizo zinahaki ya kupata mahitaji na kuzuia ni kuwahukumu. 

Hakimu Mwijage aliamuru upande wa Mashtaka na utetezi kushirikiana kulishughulikia familia hizo zipate mishahara hiyo  na Novemba ,23,2017 wapeleke taarifa.

Pia aliamuru upande wa Mashtaka siku hiyo kupeleka mahakamani hapo taarifa inayoeleweka kuhusiana na upelelezi umefikia wapi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa  kusababisha hasara ya dola za Kimarekani 1,118,291.43 sawa na Sh 2,486,397,982.54.

Kalugendo ambaye ni Mkazi wa Kinyerezi na Rweyemamu Mkazi wa Mwananyamala wote ni waajiriwa wa Wizara ya Nishati na  Madini.

Kati ya Agosti 25 na ,31, 2017 katika maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Shinyanga, washtakiwa hao kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathamini walioajiliwa na Wizara ya Nishati na Madini walisababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi. Washtakiwa wapo rumande.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search