Vigogo wanne Tanesco wafikishwa mahakamani...soma habari kamili na Matukio360..#share
Na Abdulrahim Sadiki
WAFANYAKAZI wanne wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) na wengine wawili leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu wakikabiliwa na Mashtaka 202 ya uhujumu uchumi na kusababisha
hasara ya bilioni 2.7.
Wafanyakazi hao wa Tanesco ni Mhasibu
Mwandamizi wa Mapato, Emmilian Mlowe, Assistant office Automation, Shakila
Ngella, Meneja Mwandamizi wa Fedha, Mkama Maira na Mhasibu anayeshughulikia
madeni, Yaled Jonas.
Wengine wanaokabiliwa na kesi huyo ni
Bashiru Ngella na Barnabas Massaly.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi
Mutalemwa leo amewasomea washtakiwa hao Mashtaka kwa kusaidiana na Wakili
wa Serikali,Gloria Mwenda mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria
Nongwa.
Kishenyi amedai kati ya Januari 7, 2014 na
Januari 31,2015 Dar es Salaam walikula njama ya kutenda makosa ya wizi.
Amedai katika kipindi hicho, washtakiwa,
Emilian, Shakila, Mkama na Yared wakiwa waajiliwa wa Tanesco Kinondoni wakiwa
na uwezo wa kuingia katika mfumo wa kompyuta unaojulikana kama Tansms33 kwa nia
ya kulaghai walifanya maingizo ya uongo katika mfumo huo ya kiasi cha Sh
2,746,485,545.63 wakijaribu kuonyesha zililipwa kwa Tanesco na mawakala
wa tatu kama manunuzi ya umeme wa Luku (unit).
Wakili Kishenyi na Wakili Mwenda waliwasomea
washtakiwa hao kwa kupokezana kuanzia shtaka la 3 hadi la 201 ambayo yote
ni ya wizi wa mamilioni ya fedha, fedha ambazo ni Mali ya Tanesco.
Katika shtaka la 202 washtakiwa hao
wanakabiliwa na shtaka la kusababisha hasara.
Wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi ,2014 na
Machi 31,2016 washtakiwa hao kwa matendo yao waliisababishia Tanesco kupata
hasara ya Sh 2,746,485,545.63.
Baada ya kusomewa Mashtaka hayo washtakiwa hao
hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya
kuisikiliza hadi Mahakama Kuu.
Upande wa Mashtaka alidai kuwa upelelezi wa
kesi huyo bado haujakamilika na wakaomba ipangiwe tarehe ya kutajwa.
Hakimu Nongwa aliwashauri washtakiwa hao
kuomba dhamana katika Mahakama Kuu kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu
Mahakama ya Mafisadi.
No comments:
Post a Comment