Waziri Mbarawa awataka wananchi kanda ya ziwa kujikomboa kiuchumi...soma habari kamili na Matukio...#share

Na mwandishi wetu
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wakazi wa kanda ya ziwa kutumia fursa ya uwepo wa uwanja wa ndege wa kisasa wa Geita kukuza utalii, kilimo, ufugaji na biashara ya madini ili kuhuisha uchumi wa mikoa ya  kanda hiyo na kujikomboa kiuchumi.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akipanda mti aina ya Muashoki kama alama ya kumbukumbu ya sehemu iliyowekwa jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa ndege wa mkoa wa Geita, leo.
Amesema hay oleo mkoani Geita  alipokuwa akiweka jiwe la msingi la uwanja huo katika kijiji cha Nyabilezi  na  amesisistiza kila mwananchi kuangalia namna atakavyonufaika na uwanja huo.  

“Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba usafiri wa anga unaimarika ili kurahisisha huduma ya usafirishaji wa abiria, hivyo kuvutia watalii katika vivutio mbalimbali nchini”, amesema Profesa Mbarawa.

Waziri Mbarawa amesema  katika kuhakikisha usafiri wa anga nchini unaimarika Serikali  imekarabati Viwanja vya ndege vya Mpanda, Bukoba, Tabora na Mafia na ina mpango wa kuvijenga kwa kiwango cha kisasa viwanja 11 nchini ili kuwezesha ndege mpya za Shirika la Ndege  (ATCL), kutoa huduma katika mikoa mbalimbali.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa mkoa wa Geita ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya usafiri wa anga nchini ya mwaka 2003 inayooelekeza uwepo wa uwanja wa ndege wa kisasa katika kila mkoa ili kurahisisha uchukuzi na kuchochea fursa za kibiashara na kitalii katika maeneo mbalimabali ya nchi.

Mhandisi Mfugale amesema Uwanja wa Ndege wa Geita ambao unajengwa na Kampuni ya kikandarasi ya Mayanga ambayo ni ya mzawa kwa gharama ya zaidi ya bilioni 41.

“Uwanja huu utakapokamilika utawezesha ndege kubwa aina ya Boeing 737 - 800 zenye uwezo wa kubeba abiria 100 hadi 200  kuruka na kutua, hivyo kuongeza na kurahisisha huduma ya usafiri wa anga katika Ukanda huo”, amesema Mhandisi Mfugale.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi, amesema wamejipanga kutumia uwanja wa ndege wa Geita katika kukuza utalii na biashara mkoani humo na kuahidi kuulinda uwanja huo na kutunza miundombinu yake.

Uwanja wa Ndege wa Geita wenye urefu wa Kilometa 3 na upana wa Mita 45 unatazamiwa kuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa Tatu kwa wakati mmoja pindi utakapokamilika.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search