LHRC wampinga Magufuli....soma habari kamili na matukio360...#share
Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimepinga kauli
ya rais John Magufuli kuhusu utaratibu wa utoaji wa taarifa za takwimu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na matukio360, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Dk. Helen Kijo-Bisimba amesema
takwimu hupingwa na takwimu.
“Hakuna mtu anayeruhusiwa kusema uongo na sheria zipo wazi,
lakini nimeshangazwa na kauli ya rais eti ni lazima takwimu zitolewe na NBS tu,
takwimu hupingwa na takwimu,” amesema
Dk. Kijo-Bisimba.
Rais Magufuli jana akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi
za makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma alisema NBS
ndiyo chombo pekee cha kutoa taarifa za takwimu nchini.
Pia rais
Magufuli aliwaagiza mkurugenzi wa NBS na vyombo vya dola kumchukulia hatua
za kisheria kwa mujibu wa sheria ya takwimu mtu au taasisis yoyote itakayotoa
takwimu tofauti na za ofisi hiyo.
Lakini Dk Kijo-Bisimba amesema si sahihi takwimu kuhodhiwa na
taasisi moja na kusisitiza kwamba takwimu hupingwa na takwimu nyingine na kuhoji kwa nini mtu au taasisi nyingine zinapotoa takwimu kinzani na NBS ziwe za uongo na kwamba ni vigumu kubaini zipi ni sawa.
Amesema kuwa jinai ni kutumia takwimu za ukweli kupotosha na hata NBS inaweza kupata takwimu za uongo hivyo kinachotakiwa ni mtu au
taasisi inayotoa takwimu kinzani kuonesha njia walizotumia.
“Nadhani hakuna mtu au taasisi inayoweza kuhodhi takwimu na
mtu kusema anatakwimu za uongo unajuaje?, mtu asipingwe eti kwa kufanya takwimu
zake, kinachotakiwa ni kudhithibitisha kwa kuonesha njia aliyotumia,” ameongeza
Dk. Kijo-Bisimba.
Miezi kadhaa iliyopita viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo waliingia katika mgogoro na
serikali kwa kutuhumiwa kutoa takwimu za uongo kuhusu hali ya uchumi nchini na
hadi sasa suala hilo lipo chini ya vyombo vya dola kwa uchunguzi.
Kwa mujibu wa sheria ya takwimu ya 2015, mtu anayetoa takwimu
za uongo adhabu yake ni kifungo cha miezi sita hadi miaka mitatu, au kulipa
faini kati ya milioni 1 hadi milioni 10 au adhabu zote kwa pamoja.




Nimeipenda maana hata hao NBS wanaweza kutuaminisha na takimu za uongo
ReplyDelete