LHRC wampinga Magufuli....soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimepinga kauli ya rais John Magufuli kuhusu utaratibu wa utoaji wa taarifa za takwimu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na matukio360, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Dk. Helen Kijo-Bisimba amesema takwimu hupingwa na takwimu.

“Hakuna mtu anayeruhusiwa kusema uongo na sheria zipo wazi, lakini nimeshangazwa na kauli ya rais eti ni lazima takwimu zitolewe na NBS tu,  takwimu hupingwa na takwimu,” amesema Dk. Kijo-Bisimba.

Rais Magufuli jana akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma alisema NBS ndiyo chombo pekee cha kutoa taarifa za takwimu nchini.

Pia  rais Magufuli aliwaagiza mkurugenzi wa NBS na vyombo vya dola kumchukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya takwimu mtu au taasisis yoyote itakayotoa takwimu tofauti na za ofisi hiyo.

Lakini Dk Kijo-Bisimba amesema si sahihi takwimu kuhodhiwa na taasisi moja na kusisitiza kwamba takwimu hupingwa na takwimu nyingine na kuhoji kwa nini  mtu au taasisi nyingine zinapotoa takwimu kinzani na NBS  ziwe za uongo  na kwamba ni vigumu kubaini zipi ni sawa.

Amesema kuwa jinai ni kutumia takwimu za ukweli kupotosha na hata NBS inaweza kupata takwimu za uongo hivyo kinachotakiwa ni mtu au taasisi inayotoa takwimu kinzani kuonesha njia walizotumia.

“Nadhani hakuna mtu au taasisi inayoweza kuhodhi takwimu na mtu kusema anatakwimu za uongo unajuaje?, mtu asipingwe eti kwa kufanya takwimu zake, kinachotakiwa ni kudhithibitisha kwa kuonesha njia aliyotumia,” ameongeza Dk. Kijo-Bisimba.

Miezi kadhaa iliyopita viongozi wa  Chama cha ACT-Wazalendo waliingia katika mgogoro na serikali kwa kutuhumiwa kutoa takwimu za uongo kuhusu hali ya uchumi nchini na hadi sasa suala hilo lipo chini ya vyombo vya dola kwa uchunguzi.

Kwa mujibu wa sheria ya takwimu ya 2015, mtu anayetoa takwimu za uongo adhabu yake ni kifungo cha miezi sita hadi miaka mitatu, au kulipa faini kati ya milioni 1 hadi milioni 10 au adhabu zote kwa pamoja.




About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

1 comment

  1. Nimeipenda maana hata hao NBS wanaweza kutuaminisha na takimu za uongo

    ReplyDelete

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search