Madabida aachiwa, akamatwa tena...soma habari kamili na maatukio360..#share

Na mwandishi wetu
ALIYEKUWA  Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano wamepanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi ikiwamo kusambaza dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi ' ARV’s ' na kusababisha hasara ya Sh 148 milioni.


 Kabla ya kusomewa kesi hiyo mpya ya uhujumu uchumi  namba 80 ya 2017, mahakama ilimfutia kesi iliyokuwa na mashtaka matano yanayofanana na hiyo iliyokuwa ikiwakabili awali  iliyofunguliwa mwaka 2014.

Kesi hiyo ilifutwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa baada ya Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro kuomba iondolewe mahakamani hapo chini ya kifungu cha 91 (1) kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao na mahakama ikaridhia ikaifuta.

Kesi hiyo ilikuwa katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na mashadi tisa walikuwa wamekwishatoa ushahidi wao na washtakiwa walikuwa nje kwa dhamana.
Baada ya kesi hiyo kufutwa, Madabida  ambaye ni afisa mtendaji mkuu wa kiwanda hicho na wenzake walikamatwa tena na kufunguliwa kesi hiyo mpya ya uhujumu uchumi.

Mbali na Madabida wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni 

Seif Shamte ambaye ni mkurugenzi  wa uendeshaji,  Simon Msoffe (meneja masoko) na  Fatma Shango (mhasibu msaidizi) wa Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd.

Pamoja na Sadick Materu na Evans Mwemezi ambao ni maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa.  

Wakili Kimaro alidai  kati ya Februari Mosi na Aprili 5,2011 Dar es Salaam, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kula njama kwa  kusambaza dawa bandia za kufubaza makali ya ukimwi.

Kimaro alidai kuwa  washtakiwa hao  Aprili 5, 2011 jijini Dar es Salaam waliisambazia Bohari Kuu ya kopo 7776 za dawa bandia za ARV’s zenye mchanganyiko wa dawa ya stavudin 30mg +nevirapine 200mg+lamivudine 150mg.

Dawa hizo zilizotengezwa Machi 2011 na kuisha muda wake wa matumizi Februari 2013 zilionyesha kuwa ni halali wakati si kweli.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuisambazia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kopo 4476 .

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia Dola za Marekani 98,506.08  (sawa na Sh 148,350,156 za Tanzania kwa udanganyifu baada ya kuonyesha kwamba fedha hizo ni malipo ya makopo 12252 ya dawa hizo za ARV’s.

Washtakiwa  Sadick Materu na Evans Mwemezi  wanadaiwa kuwa  kati ya Aprili 5 na 13 mwaka 2011 wakiwa maafisa wa Bohari Kuu ya Dawa walishindwa kuzuia kosa kutendekea.

Washtakiwa  hao wote, wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kutimiza wajibu na kuisababishia MSD  hasara ya Sh 148,350,156.48 kwa kusambaza dawa hizo bandia za kufubaza makali ya Ukimwi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa hao hawakurusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Wakili wa Serikali,Pius Hilla alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika lakini DPP bado hajafanya maamuzi kama ile kesi isikilizwe Kisutu ama Mahakama Kuu.

Washtakiwa hao wanatetewa na Mawakili Denis Msafiri, Makaki Masatu na Nehemiah Nkoko.

Wakili Msafiri  Alisema Mahakama ya Kisutu inayo  mamlaka ya kuisikiliza hiyo kwa sababu kiwango chake cha fedha  kipo chini ya Sh 1 bilioni  ambayo ndiyo inapaswa kusikilizwa mahakama Kuu.

Kutokana na hoja hiyo Wakili Hilla aliomba wapewe muda hadi Leo ndiyo wajibu hoja ya upande wa utetezi.

Hakimu Nongwa  aliiahirisha kesi hiyo hadi Leo kutokana na ombi hilo na kuamuru washtakiwa wapelekwe polisi hadi Leo itakaposikilizwa hoja kama mahakama hiyo inamamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ama la.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search