Mbunge akanusha kuhamia CCM....soma habari kamili na matukio360..#share

Na Abraham Ntambara,Dar es salaam

MBUNGE wa Moshi Vijini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) Antony Komu amesema hawezi kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mbunge wa Moshi Vijijini Antony Komu, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja baada ya siku kadhaa kuwepo kwa uvumi kuwa yeye ni mmoja wa wabunge wa Chadema ambao wangetarajiwa kukihama hivyo taarifa hii inahitimisha uvumi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam waziri huyo kivuli wa viwanda, biashara na uwekezaji , amesema atakuwa ni mtu wa ajabu kuhamia CCM na kuiunga mkono serikali ambayo inavunja katiba ya nchi.

“Nitakuwa ni mtu wa ajabu sana kuungana na serikali hii, kwa mtu mwenye akili timamu huwezi kuwa sehemu ya serikali hii ambayo inaminya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa siasa, tulikuwa na bunge ‘live’ lakini hii fursa imeondoshwa,” amesema Komu.

Komu amesema kuwa hajawahi kusikia wala kutumiwa ujumbe wa simu kushawishiwa kujiunga na CCM na ni kutokana na kwamba yeye hawezi kujaribiwa katika hilo hilo na kuingia katika mtego huo.

Amedai kuwa uvumi dhidi yake huenda kuwa ni propaganda zinazofanywa na chama tawala ili kuhamisha mijadala ya msingi katika nchi kama ya hali ya kudorola kwa uchumi hivyo  serikali kutumia mwanya huo kukwepa kujibu mijadala hiyo.

Amesema kuwa yeye ni mmoja wa waanzilishi wa mfumo wa vyama vingi hivyo ataonekana mtu wa ajabu kuhama chama kwani vyama vya upinzani vinahitajika ili kuikosoa serikali inapokosea ili mambo mengine yaende vizuri.

Kwa upande mwingine Komu amesema kuwa wanaohamia CCM wamekuwa wakitoa hoja dhaifu ambazo haziwezi kumsawishi mtu mwenye kujielewa.

Amesema wapo wanaohama vyama vyao kutokana na serikali kuwasumbua katika shughuli zao pamoja na kuwapa vitisho mbalimbali.

Pia amedai kuwa wanaohama ni wale waliochoka kutokana na madeni mbalimbali hivyo wanarubuniwa ili kuweza kupatiwa msaada wa  madeni yao.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search