Mwanafunzi mbaroni kwa kukutwa na sare za JWTZ...soma habari kamili na matukio360...#share
Na Salha Mohamed
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Fahari iliyopo Goba Said Selemani (17) kwa kosa la kukutwa na sare za JWTZ (Kombat).
Lazaro Mambosasa akiwa na sare za JWTZ alizokutwa nazo mwanafunzi
Mwanafunzi huyo alikamatwa maeneo ya Mbezi CRDB bank akiwa amevaa sare hizo za JWTZ huku akivuta sigara hadharani na kufanya vitendo vingine ambavyo haviendani na maadili ya askari aliyevaa sare.
Akizungmza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, SACP Lazaro Mambosasa amesema katika mahojiano ya awali kijana huyo alijitambulisha ni askari kutoka kikosi cha 501 KJ kilichopo Lugalo jijini humo.
"Baada ya kubanwa zaidi alikiri kupata sare hizo kutoka kwa rafiki zake anaokuwa nao sehemu mbalimbali,"amesema.
Amesema alipopekuliwa katika begi la mgongoni alilokuwa nalo alikutwa na kofia nyingine moja pamoja na kitambulisho namba DFF 7001A cha familia ya askari chenye namba 1231 ambacho ni cha mtoto wa askari wa JWTZ MT 65640 Private Gabriel Kihwili wa 501 KJ kikiwa na picha ya mtoto wake Elia Gabriel.
"Uchunguzi bado unaendelea ili kuwapata rafiki zake hao ambao inadhaniwa kuwa huwa wanashirikiana katika kufanya matukio ya kihalifu,"amesema.
Katika hatua nyingine,jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu waliokuwa wakijihusisha na matukio ya uporaji na mauaji mbalimbali jijini humo wakiwa na silaha aina ya AK. 47 na risasi 57.
"Baada ya mahojiano watuhumiwa hao walikubali kuonesha silaha moja aina ya AK.47, Magazine mbili (2) na risasi 57 ambayo walikuwa wameificha kwenye kichaka karibu na eneo la Ubungo Mawasiliano.
"Pia walionesha pikipiki mbili aina ya Boxer zenye namba za usajili MC 757 BCT rangi nyekundu na MC 946 BSE rangi nyeusi ambazo walizipora katika matukio mbalimbali,"amesema.
Amesema walipohojiwa walisema wanazo silaha nyingine ambazo wamezificha kwenye kichaka eneo la Ununio na wako tayari kwenda kuonyesha silaha hizo.
"Walipofika huko wakati wakishuka kwenye gari jambazi mmoja raia wa Burundi aliyefahamika kwa jina la Fanuel Luchunda Kamana alimvamia askari kwa lengo la kumpora silaha huku wenzake wawili wakijaribu kutoroka na ndipo walijeruhiwa kwa risasi,"amesema.
Mambosasa amesema majambazi hao waliwahishwa katika hospitali ya Mwananyamala ili kupatiwa matibabu na ndipo madaktari wakabaini kuwa tayari wameshafariki dunia.
Amefafanua kuwa miili imehifadhiwa hospitalini hapo kwa hatua za uchunguzi wa kitaalamu.
Amesema awali majambazi hao walikiri kufanya matukio kadhaa ya uporaji na mauaji likiwemo tukio la mauaji huko Kunduchi Mtongani lililotokea Novemba /2017 ambapo uuwa madereva bodaboda na kupora pikipiki zao na kuziuza kwa sh.800, 000.
"Majambazi wengine waliofariki ni Gallus Marandu Clement (31) na Fredrick Wilbroad Achalo mkazi wa Gongo la Mboto,"amesema.
Ameongeza kuwa Novemba 11/2017 jeshi hilo walikamata gari aina ya Ipsum lenye namba T. 142 CNF na radio call aina ya motorola maeneo ya Mbezi Msumi pamoja na kamba za katani na vipande viwili vya nondo vilivyokuwa vikitumiwa na kundi la majambazi wapatao watano waliokuwa wamevamia katika nyumba ya Erick Mkwemwa.
"Awali majambazi hao wapatao watano walifika katika nyumba hiyo na kujitambulisha kuwa wao ni maofisa wa Polisi waliofika hapo kwa ajili ya kufanya upekuzi lakini badala yake waliwaweka chini ya ulinzi familia hiyo na kuwafunga kamba mikononi,miguuni kisha kuwaziba na plasta mdomoni na hatimaye majirani wa eneo hilo walitilia mashaka kitendo hicho na kuamua kuizingira nyumba hiyo huku wakitoa upepo matairi ya gari,"amesema.
Amesema majambazi hao walipobaini kitendo hicho walianza kukimbia huku wakifukuzwa na wananchi ambapo wawili kati yao walikamatwa na kuanza kushambuliwa kwa kupigwa fimbo/mawe na hatimaye walifariki dunia huku wengine watatu wakifanikiwa kutoroka.
"Miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili huku msako mkali ukiendelea ili kuwakamata majambazi wengine 3 waliokimbia,"amesema.
Ameongeza kuwa, jeshi hilo lilifanikiwa kumuuwa jambazi sugu aliyetumia bastola feki(Iliyotengenezwa kienyeji) katika kupora pikipiki mwenye umri Kati ya miaka 25-30.
"Awali jambazi huyo alimkodi dereva pikipiki ili ampeleke maeneo ya Msitu wa Jeshi huko Buza lakini ghafla walipofika maeneo hayo jambazi huyo alitoa bastola yake iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na baruti na kumuamuru dereva ashuke na kumuachia pikipiki,baada ya kushuka dereva alipiga kelele kuomba msaada na ndipo wananchi walijitokeza na kuanza kumpiga kwa mawe huku wengine wakimkata mapanga,"amesema.
Amesema askari walipata taarifa na walipofika eneo hilo walimkuta jambazi huyo akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na ndipo walimkimbiza katika hospitali ya Temeke kwa ajili ya matibabu na muda mfupi baadae alifariki dunia.
Ameeleza kuwa jeshi hilo lilikamata bajaji yenye namba za usajili MC 473 BMM rangi ya blue iliyoibwa Kigamboni Mjimwema nyumbani kwa Chandra Kandri.
"Baada ya askari kupata taarifa ya kupotea kwa bajaji hiyo ufuatiliaji ulianza mara moja na ndipo Bajaji hiyo ilipatikana huko Sumbawanga mkoani Rukwa ikiwa imetelekezwa na watu wasiojulikana baada ya kushindwa kufanya zoezi la kubadilisha umiliki wake,"amesema.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment