Tundu Lissu: Nilipoteza fahamu wiki mbili...soma habari kamili na matukio360..#share

 Na mwandishi wetu, Nairobi

MWANASHERIA mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye amekuwa akipokea matibabu Nairobi tangu alipopigwa risasi na watu wasiojulikana mkoani Dodoma mwezi Septemba, amesema  alipoteza fahamu wiki mbili.

Tundu Lissu akiwa hospitalini mjini Nairobi, Kenya akipatiwa  matibabu

Akizungumza katika mahojiano maalum na matukio360, mbunge huyo wa Singida Mashariki pia amesema anaamini kushambuliwa kwake kulihusiana na siasa.
Akisimulia jinsi tukio la kupigwa kwake risasi lilivyokuwa Tundu Lissu amesema ; ‘’Tulipofika karibu  na nyumbani mara niliona gari aina ya Land Cruiser Prado lenye rangi nyeupe likisimama  pembeni yetu kuelekea mahala tulipotokea, akashuka mtu mmoja, akaenda kuzungumza  mlango wa mbele mara wakashuka watu wawili wembamba wakiwa wamevalia kofia za kufunika sura zao  wameshika ‘Shot Gun’.
‘’Mara nikasikia mlipuko puu, baada ya hapo nikashtukia nipo Hospitalini Nairobi yaani nilipoteza fahamu kwa wiki mbili.’’

Kuhusu mwenendo wa afya yake amesema  anaendelea kupata nafuu na muda si mrefu hali yake itatengemaa na kuwa imara.  

Pamoja na mambo mengine amelilaumu Bunge la Tanzania akisema halijachukua hatua zozote kumsaidia tangu kulazwa kwake hospitalini.
Hata hivyo amemshukuru makamu wa rais Samia Suluhu na rais mstaafu Ally Hassan Mwinyi kwa kumtembelea hospitalini hivi karibuni.

Bunge la Tanzania  limeshatoa ufafanuzi kuhusu suala hilo na kwamba linafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Lissu ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani alipigwa risasi zaidi ya thelathini na watu ambao mpaka sasa hawafahamiki pindi alipokuwa mjini Dodoma akihudhuria vikao vya bunge.

Jeshi la polisi nchini lilisema upelelezi wa tukio hilo unasuasua kutokana na dereva wa Mbunge huyo kutofika polisi kutoa ushahidi.

Hata hivyo, taarifa kutoka Chadema zilisema  dereva wa mbunge huyo yuko nchini Kenya kwa ajili ya kupata matibabu ya kisaikolojia kutokana msongo wa mawazo alioupata baada ya kisa hicho.


Lissu yuko nchini Kenya kwa takribani miezi mitatu sasa ambako anapatiwa matibabu kutokana na majeraha ya risasi aliyoyapata kutokana na shambulio hilo.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search