Wanahabari wataka Bunge, wanasiasa kutoa tamko upoteaji watu kiholela...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Salha Mohamed
WADAU wa usalama wa wanahabari wamewataka viongozi wa siasa na Bunge kujadili utekaji na kupotea kwa wananchi nchini na kutoa maazimio.
Mwenyekiti wa MCT, Kajubi Mukajanga
Mwenyekiti wa MCT, Kajubi Mukajanga
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kutoweka kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda(42)na kulaani tukio hilo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, wakati akitoa tamko la pamoja Mwenyekiti wa Baraza la Habari(MCT),kajubi Mukajanga amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuhakikisha kila raia anaishi kwa uhuru na usalama nchini.
"Azaki, vyombo vya habari na umma wa watanzania wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vyovyote ambavyo vinalenga au kuashiria kuzuia uhuru wa maoni nchini...leo ni Azori na wengine haijulikani siku wala saa ya kutekwa wala kupotea kwa mwandishi mtetezi au raia wa kawaida, "amesema.
Amesema kutokana na wimbi la utekaji na kutoweka kwa wananchi serikali inapaswa kutia sahihi na kuridhia mkataba wa kimataifa kwa ajili ya ulinzi wa watu wote waliotekwa na kuwekwa vizuizini pamoja na mkataba wa kimataifa wa kuzuia utesaji na vitendo vya vingine vya kikatili vinavyotweza utu wa binadamu.
"Watetezi wa haki za binadamu tuungane na kupaza sauti zetu kwa pamoja juu ya hali ya watu kutoweka inayozidi kushika kasi nchini, "amesema.
Amewataka wananchi kushirikiana kuwafichua watu wenye nia ya kuwaangamiza watanzania wenzao bila hatia yeyote.
Akizungumzia shuhuda mbalimbali za kutoweka kwa Gwanda, Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu (THRDC), onesmo Olengurumwa amesema walizungumza na Kamanda wa polisi mkoani pwani ambapo alikiri kupotea kwa mwandishi huyo.
Amesema kamanda huyo alikaririwa akisema"kwakuwa ndugu Azory Gwanda alimuaga mke wake kwamba anaenda safarini na atarudi huenda ni kweli atarudi,"amesema.
Amesema kwakuwa suala hilo limesharipotiwa polisi wataendelea kulifanyia kazi na endapo watapata taarifa zitakazoweza kusaidia kupatikana kwake wataufahamisha umma na mke wake.
Azory ametoweka tangu Novemba 21,2017 ambapo hajapatikana hadi leo.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment