3000 wajitokeza kwa Makonda...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam


ZAIDI ya wananchi 3000 wanaodaiwa kudhulumiwa mali zao jijini Dar es Salaam  wamejitokeza kupata utatuzi wa malalamiko ya kisheria kwa mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda.
Baadhi ya wananchi wa Dar es salaam wakiwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, wakipatiwa msaada wa kisheria wa mali zao mbalimbali walizodhulumiwa

Wananchi hao watapatiwa msaada wa kisheria kwa wanasheria magwiji 160 ikiwa ni mkakati wa  Makonda kusaidia wanyonge waliodhulumiwa mali zao kupata haki pasipo kuvunja sheria.


Makonda amesema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza jana inatoa picha kamili kuwa wapo viongozi wasiotekeleza vyema majukumu yao ya kiofisi kwenye idara zao ambapo ameahidi kuwawajibisha.


Amesema kilichomgusa kuandaa wiki ya msaada wa kisheria ni baada ya kubaini uwepo wa wananchi wanaonyanyasiki na hata kufikia hatua ya kufa kwa presha au kupooza miili baada ya kudhulumiwa na watu wenye pesa au wanaotumia uelewa wa sheria kukandamiza wanyonge.


Kutokana na idadi kuwa kubwa wanaoendelea kujitokeza, Makonda ataongeza wanasheria  zaidi ili kuhakikisha kila anaefika na kupata namba anahudumiwa ipasavyo ambapo amewaomba wanasheria kuhakikisha wanawasikiliza wananchi kwa umakini na kuchambua nyaraka kwa ufasaha na wasitoe hukumu.


Makonda amesema mchakato huo umehusisha wanasheria wabobezi, wataalam wa kutambua nyaraka zilizogushiwa, watendaji wa ardhi na watumishi wa Mahakama ambao wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.


Makonda amesema baada ya kupokea ripoti kamili ya kesi zote atasimama kuhakikisha hakuna mnyonge anabaki akinyanyasika.


Mchakato wa kusikiliza wananchi waliodhulumiwa mali zao ikiwemo nyumba, viwanja, magari, mirathi na kazi litaendelea hadi siku ya Ijumaa ya Februari 02.


Kwa upande wa wananchi waliojitokeza wamemshukuru Makonda kwa kutambua tabu wanazozipata baada ya kudhulumiwa na wajanja ambapo wengine wamesema wamepoteza waume, wake zao na wengine kupata magonjwa baada ya kudhulumiwa.


Wamesema  wametaabika muda mrefu kutafuta haki pasipo kufanikiwa lakini kupitia utendaji kazi makini wa Makonda wanaamni haki inapatikana.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search