Halmashauri Mufindi yatoa milioni 100 kwa vikundi...soma habari kamili na matukio360...#share
Na Mwandishi Wetu, Mufindi
JUMLA ya shilingi milioni 100, zimetolewa kwa sharti la mkopo kwa vikundi vya Wanawake na Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, ikiwa ni utekelezaji wa takwa la sheria inayozitaka mamlaka za Serikali za mitaa nchini kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa lengo la kuwakopesha vijana na Wanawake ili wajiajiri kupitia shughuli za kijasirimali hivyo kuboresha maisha yao.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William akikabidhi mfano wa hundi kwa afisa wa benki, kama ishara ya kuruhusu utoaji mikopo.
Akisoma taarifa ya mikopo hiyo, mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Hatibu Bwashehe amesema kuwa, kati ya vikundi hivyo, vikundi 22 vya wanawake vimekopeshwa jumla ya shilingi milioni 62, wakati vikundi 15 vya Vijana vimenufaika na Mkopo huo kwa kupata shilingi Milioni 38.
Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi kwa walengwa, mgeni wa rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri William, amevitaka vikundi hivyo vielewe kuwa, fedha wanazopokea ni Mkopo hivyo, zitumike kulingana na maandiko waliyowasilisha badala ya kuzitumia kwa malengo tofauti kama vile kuchangia harusi au kununua mavazi ya kifahari na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa kutorejesha fedha za Serikali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Festo Ngina amepongeza mwenendo mzuri ya urejeshaji Mikopo kwa vikundi vilivyokopeshwa kiasi cha shilingi milioni 300 kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2016/2017 na akaongeza kuwa ili hali ya urejeshaji izidi kuwa bora zaidi, watendaji wa Kata na Vijiji watahusika kufuatilia marejesho hayo kama ambavyo wanahusishwa kwenye chakato kusajili vikundi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtendaji wa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Profesa Riziki Shemdoe amewahimiza vijana na Wanawake wa Halmashauri hiyo kuendelea kuwasilisha maombi kwa kuwa Halmashauri yake tayari imetenga fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni 140 ambazo watazikopesha baadaye mwezi ujao mara baada ya kukamilisha uchambuzi wa maandiko ambayo yatakuwa yanalenga kuanzisha viwanda Vidogo.
Aidha, wanufaika wa Mkopo huo ambao ni Wanawake na Vijana, wameipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli, kwa kuwathamini na kuwapatia mikopo hiyo huku wakiahidi kuzitumia kwa malengo na kurejesha kwa wakati.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment