Jalada kesi mhasibu Takukuru lapelekwa Takukuru ...soma habari kamili na matukio 360...#share

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

JALADA la kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zisizoendana na kipato chake  inayomkabili aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake watatu limepelekwa Takukuru kwa ajili ya upelelezi zaidi.
Aliyekuwa mhasibu wa Takukuru, Godfrey Gugai akitoka katika chumba cha mahakama ya hakimu mkazi Kisutu leo jijini Dar es salaam.

Wakili wa Serikali Simon Wankyo akisaidiana na wakili Salim Msemo ameeleza leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa upelelezi ikiwa haujakamilika.

Wakili Wankyo amedai, jalada la kesi hiyo lilipelekwa kwa  Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP) kwa ajili ya kusomwa na sasa limerudishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa ajili ya upelelezi zaidi.

Ameongeza, baada ya kukamilisha upelelezi, jalada hilo litarudishwa tena kwa DPP ili kujiridhisha kama maelekezo aliyoyatoa yamefanyiwa Kazi.

Hata hivyo, baada ya maelezo hayo, wakili wa Utetezi Alex Mshumbusi alidai kuwa hategemei upelelezi kuchukua muda mrefu kwa sababu mshtakiwa Gugai alikuwa mtumishi wa Takukuru na tayari alishashtakiwa kinidhamu na Takukuru yenyewe na kupoteza ajira yake.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 31, mwaka huu itakapotajwa.

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.Washitakiwa hao wanaokabiliwa na mashitaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.


Katika shitaka la kwanza ambalo ni kumiliki mali ambazo hazina maelezo ambalo linamkabili Gugai, inadaiwa kati ya January 2005 na December 2015, jijini Dar es Salaam, akiwa ofisa wa umma ameajiriwa na TAKUKURU anamiliki mali zenye thamani  zaidi ya Sh 3.6bilioni  ambazo haziendani na kipato chake cha sasa wala cha nyuma.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search