Daraja Ruhuhu kukamilika mwezi Juni...soma habari kamili na matukio 360...#share
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
NAIBU Waziri wa
Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka mkandarasi anayejenga daraja la Ruhuhu
wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili
kuhakikisha anamaliza daraja hilo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa na kwamba ifikapo mwezi Juni,2018 akabidhi.
Meneja wa Wakala wa
Barabara (TANROADS), mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Lazeck Alinanuswe (katikati),
akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa Daraja la Ruhuhu lililopo wilayani Nyasa,
mkoani humo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati alipokagua daraja hilo kuona maendeleo ya ujenzi wake.
Agizo hilo
amelitoa leo Wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma alipokuwa akikagua ujenzi wa daraja
hilo ambapo ameusisitiza Uongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Makao
makuu kuhakikisha kuwa utaratibu wa zoezi zima la ununuzi wa vyuma vitakavyowekwa
juu ya daraja hilo linaenda sambamba na makadirio ya muda wa mradi ili
kupelekea kazi hiyo kukamilika kwa muda uliopangwa.
"Nafikiri
sasa jipangeni vizuri ili masika yakiiisha mhakikishe mnafanya kazi kwa bidii
ya hali ya juu, nataka kufikia mwezi Juni daraja liwe limekamilika, pia
TANROADS Makao makuu hakikisheni mchakato wa manunuzi ya vyuma vya daraja
mnauanza mapema ili kuweza kukamilika mapema, msisubiri hadi daraja hili
kukamilika", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Ameongeza kuwa
daraja hilo likikamilika litakuwa ni kiungo kwa watu wa Nyasa mkoani Ruvuma na
Ludewa mkoani Njombe kwani wamekuwa wakilisubiri daraja hilo kwa ajili ya
kujiendeleza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Aidha,
amemwagiza Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani humo, Mhandisi
Elisha Mgira, kuhakikisha anarekebisha kasoro zilizopo kwenye kivuko cha Ruhuhu
ili kuweza kufanya kazi katika kipindi hiki ambacho wananchi wanasubiri ujenzi
wa daraja kukamilika.
Kwa upande wake,
Mhandisi Mkazi wa daraja hilo, Mhandisi Napegwa Kiseko, amesema kuwa Ujenzi wa
mradi huo umefika asilimia 50 ambapo kazi zinazofanyika sasa ni kujaza matabaka
ya barabara zinazoingia darajani hapo ili kunyanyua tuta la barabara.
Amefafanua kuwa
kazi hiyo inaendelea pande zote mbili yaani mkoa wa Ruvuma na Njombe
ingawa kwa kipindi hiki cha mvua kazi hiyo imekuwa na vikwazo vingi.
"Ujenzi wa
misingi ya daraja kwa upande wa mkoa wa Ruvuma upo kwenye hatua za mwisho na
kwa upande wa Njombe ujenzi wa misingi ulianza mwishoni mwa mwezi Disemba na unaendelea",
amesisitiza Mhandisi Kiseko.
Mradi wa ujenzi
wa daraja la mto Ruhuhu ambao upo mpakani mwa mkoa wa Ruvuma na Njombe
unatarajiwa kugharimu takribani kiasi cha shilingi Bilioni 6 ambazo ni
fedha za Serikali kwa asilimia mia moja na unatarajiwa kukamilka mwezi Juni
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment