Kesi inayomkabili Mattaka kuunguruma Februari ....soma habari kamili na matukio360...#share

 Na mwandishi wetu, Dar es salaam
KESI ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kusababisha hasara kupitia ukodishaji ndege inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka na wenzake wawili itaendelea  kuunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Februari 22,2018.


Kesi   hiyo  leo  imeahirishwa  kwa Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri hadi Februari 22,2018 ambapo mashahidi wa  upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi  wao.

Mbali na Mattaka washtakiwa wengine wanaokabiliwa katika kesi hiyo, inayoendeshwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter  mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, ni  Afisa Mtendaji Mkuu Mstaafu wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA),  Ramadhan Mlinga na  Mwanasheria wa mamlaka hiyo,  Bertha Soka.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 9,2007 katika ofisi za ATCL zilizopo wilayani  Ilala, Mattaka  wakati akitekeleza majukumu yake alitumia vibaya madaraka yake kwa kutia saini kwenye mkataba wa ukodishaji wa ndege  A 320-214  iliyotengenezwa kwa  namba 630 baina ya Wallis Trading Inc na ATCL.

 Mattaka anadaiwa kuwa alifanya hivyo  bila ya kuzingatia sheria ya Manunuzi ya Umma na  kutofuata taratibu za zabuni kwenye  mchakato wote.

Mkurugenzi  Mtendaji huyo wa zamani  wa ATCL, Mattaka anadaiwa kuwa Oktoba 27,2007 alitumia vibaya madaraka yake kwa kutia saini kwenye cheti cha kuruhusu mchakato wa ukodishaji wa h ndege hiyo  bila ya kufuata ushauri wa kiufundi aliokuwa amepatiwa.

 Mattaka anaendelea kudaiwa kuwa kati ya Oktoba 27,2007 na Aprili 24,2008  kwenye ofisi za ATCL  kutokana na kitendo chake cha kutia saini cheti hicho bila ya kuzingatia ushauri wa kiufundi  alisababisha hasara ya dola za Kimarekani 772,402.08 zilizolipwa kwa kampuni ya  Aeromantenimiento , S. A kama gharama  za huduma ya matengenezo.

Kati ya Oktoba 27 na Novemba 29,2007 kwenye ofisi hizo za ATCL, Mattaka anadaiwa kutia kwake saini kwenye cheti hicho kulisababisha hasara  ya dola za Kimarekani 35,984.82 ambazo  zilizolipwa kwa kampuni ya Lantal Textiles, INC kwa ajili ya ununuaji wa mahitaji ya ndege hiyo ikiwamo Kapeti.

Iliendelea kudaiwa kuwa, kati ya Oktoba 9, 2007 na Oktoba 26, 2011, kutokana na kitendo cha Mattaka  kutia saini  kwenye mkataba baina ya kampuni  ya Wallis Tranding Inc ya Liberia na ATCL alisababisha hasara ya dola za Kimarekani 42,459,316.12 ambazo ATCL iliilipa kampuni hiyo.

Kwa upande wa washtakiwa Mlinga na Bertha, wao wanadaiwa kuwa Machi 19,2008 katika ofisi za PPRA  zilizopo wilaya ya Ilala kwa nia ya udanganyifu walighushi Muhtasari wa kikao cha siku hiyo  wakionyesha  mamlaka hiyo ilifanya kikao cha kujadili maombi  ya ATCL juu ya kuidhinishwa kwa mkataba huo.  Washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search