Ruvuma walilia barabara ...soma habari kamili na matukio360....#share
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
WANANCHI wa Mbamba Bay
wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara
ya Mbinga-Mbamba Bay (km 67), kwa kiwango cha lami ili kutatua changamoto za
usafirishaji wa abiria na mizigo wanazozipata hususan katika kipindi cha
masika.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya
kukagua miradi ya ujenzi wa jengo la ofisi na nyumba ya makazi ya Mkuu wa
Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma. Miradi hiyo inajengwa na Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA).
Wananchi hao wametoa
kero hiyo mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, alipofika wilayani
hapo kukagua barabara hiyo ambapo wamefafanua kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa na
maliasili nyingi, wawekezaji na wafanyabiashara hushindwa kufika kutokana na
changamoto ya barabara, hivyo kupelekea uchelewaji wa maendeleo katika wilaya
yao.
"Uduni wa barabara
hii unapelekea kutopata maendeleo ya haraka, pia usafiri kutoka hapa kwenda
maeneo mengine ya jirani huwa mgumu hususan katika kipindi cha mvua kwani
madereva wengi hupandisha nauli", amesema mmoja wa wakazi wa Mbamba Bay, Bw.
Bahati Ndege.
Aidha, wananchi hao
wameipongeza Serikali kwa hatua zinazofanya katika utatuzi wa kero mbalimbali
zinazowakabili, hivyo wamefafanua kuwa Serikali kuamua kujenga barabara ya lami
kutaboresha uchumi katika wilaya yao na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri Elias Kwandikwa, amesema kuwa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo
umesainiwa tangu Mwezi Desemba mwaka jana na kufafanua kuwa kinachosubiriwa
sasa ni kwa mkandarasi kufika eneo la mradi na kuleta mitambo yake.
"Kila kitu kipo
tayari, Wananchi wasubiri kwa hamu ujenzi wa barabara hii ambao unatarajiwa
kujengwa kwa shilingi bilioni 129 na mkandarasi CHICO kwa ufadhili wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Amepongeza uongozi wa
Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani humo kwa kuweka changarawe katika
barabara hiyo ambapo kwa namna moja inasaidia kurahisisha usafiri kwa kipindi hiki
ambacho mkandarasi anasubiriwa kufika eneo la kazi.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri huyo amekagua mradi wa ujenzi wa Ofisi na Nyumba ya Makazi ya Mkuu
wa Wilaya ya Nyasa zinazojengwa na Wakala wa Majengo (TBA), mkoani humo na kuridhishwa
na kasi ya ujenzi wake.
Naye, Meneja wa TBA
mkoani humo, Mhandisi Edwin Nunduma, amesema kuwa TBA katika wilaya hiyo ina
jumla ya miradi minne inayoendelea kwa sasa ikiwemo mradi wa ujenzi wa
zahanati, nyumba na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo amemhakikishia Waziri huyo
kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Naibu Waziri Kwandikwa
ameanza ziara ya kikazi mkoani Ruvuma ambapo leo amekagua miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Wizara yake ili kujionea maendeleo yake.
No comments:
Post a Comment