Taasisi ya moyo JKCI yaokoa milion 800....soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham  Ntambara, Dar es Salaam

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wiki moja imeokoa sh.milioni 800 ambazo zingetumika kwenye upasuaji wa bila kufungua kifua  (Catheterization) kwa watoto 15 wenye matatizo ya moyo.
Katikati ni Mkurugenzi wa Matibabu ya Moyo wa JKCI Dk. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Fedha hizo zingetumika kwenye upasuaji wa watoto hao kama wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Matibabu ya Moyo wa JKCI Dk. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upasuaji wa bila kufungua kifua kwa watoto hao.

Amesema upasuaji huo ulifanywa na taasisi hiyo kwa kushirikiana  na taasisi ya okoa moyo wa watoto (save a child’s hesrt-sach) ya nchini Israel na kituo cha moyo cha Berlin (Berlin Heart Center) cha nchini Ujermani.

“Upasuaji huu unatumia mtambo wa Cathlab umefanyika katika kambi maalum ya matibabu iliyoanza Januari 20 hadi 25, 2018. Matibabu yaliyofanyika ni kuzibua matundu kwenye moyo na kutanua mishipa ya moyo kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 18,”

“Na kwa upasuaji huu tumeokoa sh. milioni 800 ambazo zingetumika kama watoto hawa wangepelekwa kuhudumiwa nje,” amesema.

Dk.  Kisenge amesema kambi hiyo ilienda sambamba na uchunguzi wa moyo kwa watoto 32 ambapo watoto 20 watafanyiwa matibabu katika kambi hii na wengine 12 waliobaki watatibiwa na madaktari wa JKCI kuanzia wiki ijayo.

Amesema kuwa wamepanga kufanya matibabu kwa watoto 20 na wanaamini hadi kambi itakapomalizika watoto hao watakuwa wamepata matibabu.

Ameongeza kuwa kambi hiyo imeenda sambamba na utoaji wa elimu ya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa watoto na jinsi ya kuwahudumia watoto walipofanyiwa upasuaji huo.

Amewaomba wazazi na walezi kutosahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa watoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni.

Kwa upande wake Profesa wa Magonjwa ya Moyo kutoka kituo cha moyo cha Berlin Protex Felix, amesema haoni sababu ya nchi kupeleka wagonjwe kutibiwa nje kwani kunawataalamu wa ndani wanaoweza kufanya hivyo.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search